Habari

Kamishna awaonya wanasiasa wanaotaka kuchafua Kazi Mtaani

July 16th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na WINNIE ATIENO

WANASIASA katika Kaunti ya Mombasa wamelaumiwa kwa kushurutisha machifu kuwaajiri vijana kutoka maeneo yao kwenye mradi wa serikali kuu maarufu Kazi Mtaani.

Kamishna wa Mombasa Gilbert Kitiyo amewaonya wanasiasa dhidi ya kuingilia mradi huo na badala yake kuacha kamati iliyotwikwa jukumu hilo na machifu kutekeleza wajibu wao.

Bw Kitiyo pia aliwahakikishia wakazi kwamba wanasiasa hawatoruhusiwa kuingilia usajili wa ajira ya Kazi Mtaani.

“Wale vijana wanaotoka katika familia fukara na kina mama watanufaika na ajira hii. Tumewasiliana na wanasiasa na kuwasihi wawaache machifu na kamati itekeleze jukumu lao. Haina haja waje na orodha ya majina ya watu wao ilhali wote hao ni watu kwenye sehemu yake,” alisema Bw Kitiyo.

Vijana wamekuwa wakiandamana wakilalamika kuhusu usajili kwenye ajira hiyo wakiwalaumu wanasiasa kuingilia mpango huo.

Hata hivyo, Bw Kitiyo aliwahakikishia wakazi kwamba swala hilo limetatuliwa.

Takriban vijana 16,758 kaunti ya Mombasa wamenufaika kwenye mpango huo awamu ya kwanza na ya pili ambayo inaanza wiki hii.

Watafanya kazi ya kudumisha mazingira bora kwa siku 11 kwa mwezi huku wakilipwa Sh455 kwa siku.

“Tunaangalia umri wao; wanaume wasipite umri wa miaka 35 nao wanawake 40. Hizi ni fedha ambazo zitasaidia familia nyingi kujimudu,” alisema Bw Kitiyo akiongea kwenye mahojiano na kituo cha rrdio mjini Mombasa.?