Habari

Kampeni zachacha Malava baada ya IEBC kupata vinara

Na SHABAN MAKOKHA July 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KAMPENI za kuwania kiti cha ubunge cha Malava katika uchaguzi mdogo ujao zimeshika kasi wiki moja baada ya uteuzi wa mwenyekiti na makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Kiti hicho kilisalia wazi kufuati kifo cha Malulu Injendi mnamo Februari 17, 2025.

Ushindani sasa ni kati ya wagombeaji wa vyama vya United Democratic Movement (UDA), Democracy for Citizen’s Party (DCP) na kile cha Democratic Action Party of Kenya (DAP-K).

Kiti hicho kimevutia zaidi ya wawaniaji 30. Hata hivyo, kuna wachache ambao wako kifua mbele na ndio wanaopigiwa upatu na vyama vyao pamoja na raia.

Wale walioko mstari wa mbele ni Wakili Edgar Busiega (DCP), Seth Panyako (UDP), mwanawe marehemu Malulu, Ryan Injendi (UDA), Caleb Sunguti (Roots), Mwalimu Mkuu mstaafu Enock Andanje (UDA), wakili Leornard Shimaka (UDA), Simon Kangwana (UDA) na Wilberforce Tuvei wa DAP-K.

Marehemu Malulu alishinda kiti hicho katika uchaguzi mkuu wa 2022 kwa tiketi ya Chama cha Amani National Congress (ANC) kilichoongozwa na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi. Marehemu Malulu alikuwa akihudumu kwa muhula wa tatu kama Mbunge wa Malava.

Naibu Kiongozi wa DCP, Cleophas Malala, juzi alimzindua mgombeaji wa chama hicho Bw Busiega katika mkutano uliofanyika nyumbani kwake katika Kabras Mashariki Jumamosi wiki iliyopita.

Bw Malala aliahidi kwamba kiongozi wa chama hicho Rigathi Gachagua atafanya mkutano mkubwa wa kisiasa kumpigia debe mgombeaji huyo wa DCP baada ya yeye kurejea nchini kutoka Amerika.

Seneta huyo wa zamani wa Kakamega alisema chama cha DCP, japo ni kipya, kimejitolea kupambana vikali na vyama vingine vilivyoundwa zamani.

“Tayari tuko na wagombeaji wawili katika maeneo bunge ya Malava na Banisa. Tunaamini kuwa watatuletea ushindi. Hapa Malava tuko na Bw Busiega ilhali kule Banisa tuko na Muhamed Aden,” akasema Bw Malala.

Bw Busiega amekuwa wakili wa ANC katika uchaguzi mkuu wa 2022 na alijiunga na chama cha DAP-K chake Eugene Wamalwa baada ya ANC kuvunjwa na wanachama wake kujiunga na chama cha UDA.