Kanjo wakunja mkia kuhusu jaribio la kufunga duka la Naivas kwa madai ya bidhaa zilizoharibika
IMEKUWA vuta nikuvute kati ya duka la jumla la Naivas na serikali ya Kaunti ya Nairobi kuhusu kufungwa kwa mojawapo ya tawi lake kwa tuhuma za kuuza ‘bidhaa zilizoharibika’.
Mapema Jumatano Mei 14, 2024, Mwenyekiti wa kamati ya Afya, Maurice Ochieng pamoja na madiwani wengine walitembelea Naivas tawi la Moi Avenue kufanya ukaguzi na kusema kuwa tawi hilo linafaa kufungwa kwa kuuza bidhaa zilizoharibika.
Baada ya saa kadhaa, duka hilo lilitoa taarifa kwa vyombo vya habari likikana madai hayo huku likisema kuwa linajitahidi kuhakikisha kuwa wateja wanapata bidhaa bora.
“Tungependa kujulisha umma kuwa yale yanayoenezwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu duka letu ni uvumi tu. Hakuna bidhaa iliyoharibika iliyopatikana katika duka letu na hakuna tawi lolote la duka letu lililofungwa kama inavyosambazwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii,” duka hilo lilisema kupitia taarifa kwa vyombo vya habari.
Baadaye mwendo wa jioni Jumatano, serikali ya Kaunti ya Nairobi kupitia afisa wa kaunti anayesimamia masuala ya afya Tom Nyakaba alitoa taarifa nyingine akisema kuwa duka hilo halifai kufungwa kwani kuna ukaguzi mwingine uliofanywa na kuonyesha kuwa kila kitu kiko sawa.
“Serikali ya Kaunti ya Nairobi ingependa kujulisha umma kuwa haikutoa agizo duka la jumla la Naivas lifungwe kama ilivyoripotiwa hapo awali wakati wa ukaguzi ulioongozwa na kamati ya kaunti inayosimamia sekta ya afya,” barua hiyo ilisoma.
Kulingana na barua hiyo iliyotiwa saini na Bw Nyakaba, Afisa anayesimamia masuala ya mazingira na usafi Anthony Muthemba alifanya ukaguzi mwingine na matokeo yalikuwa tofauti.
“Afisa huyo aliona kuwa masuala yalioibuliwa hayakufaa kufikia kwa hatua ya tawi la duka hilo kufungwa. Kulingana na matokeo hayo, serikali ya kaunti ya Nairobi imeamua duka hilo liendelee kutoa huduma huku barua hitajika zikikaguliwa katika ngazi ya juu.”