Karani wa Seneti kulipwa Sh10.5 milioni kwa kuchafuliwa jina na aliyekuwa Seneta Orwoba
MAHAKAMA imeagiza aliyekuwa Seneta Gloria Orwoba amlipe Karani wa Seneti Jeremiah Nyegenye Sh10.5 milioni kwa kumchafulia jina mitandaoni.
Bi Orwoba alikuwa amemlaumu Bw Nyegenye kwa unyanyasaji wa kingono, madai ambayo karani huyo wa Seneti alikanusha vikali na ndipo akaenda mahakamani.
Pigo hili linamjia Bi Orwoba muda mfupi tu baada ya kutimuliwa kama Seneta Maalum.
Hakimu wa Mahakama ya Biashara ya Milimani, Ruguru Ngotho, katika hukumu iliyotolewa Julai 14, 2025, aliamua kuwa matamshi ya Bi Orwoba yaliyochapishwa katika mitandao yake ya kijamii yalikuwa ya kumharibia jina na yenye nia mbaya na hayakuwa na kinga ya bunge kama alivyodai.
Machapisho hayo yaliyojaa chuki na madai yasiyo na ushahidi yalichapishwa kwenye WhatsApp, ukurasa wake wa Facebook na akaunti yake ya X (zamani Twitter).
Katika hukumu ya kina, Hakimu Ngotho alimwamuru seneta huyo wa zamani kuomba msamaha rasmi kwa Bw Nyegenye kupitia mitandao hiyo hiyo ya kijamii pamoja na gazeti la kitaifa ndani ya siku 30, la sivyo atalipa fidia ya ziada ya Sh1 milioni, ambayo pia itaanza kutozwa riba baada ya siku 30 kwisha.
Zaidi ya hayo, yeye binafsi au kupitia maajenti au wanablogu wake, amekatazwa kabisa kuchapisha tena matamshi yoyote dhidi ya Karani huyo wa Seneti.
“Mshtakiwa atamlipa mlalamishi Sh8 milioni kama fidia ya jumla; na Sh2.5 milioni kama fidia ya adhabu na fidia ya uovu alioonyesha.”
“Mshtakiwa atalipa riba kwa makosa haya kuanzia tarehe ya hukumu hadi malipo kamili. Mlalamishi pia atalipwa gharama za kesi. Imeamriwa hivyo,” ilisema hukumu hiyo.