Karua: Kuna njama ya kunyima Gen Z vitambulisho wasipige kura
KIONGOZI wa Narc-Kenya Martha Karua amedai serikali inaendeleza njama ya kunyima vijana nafasi ya kupata vitambulisho vya kitaifa kwa lengo la kuwazuia kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa 2027.
“Kuna njama ya kuzima Gen Zs wasijisajili kuwa wapiga kura. Tunataka vijana wapewe vitambulisho vipya bila malipo na usajili wa wapiga kura na zoezi la usajili wa wapiga kura uendelee. Wakenya wote wako na haki ya kuchagua viongozi wanaowataka bila kudhibitiwa,” akasema.
Bi Karua alilalamika kuwa vijana wanalazimishwa kulipa ada ya Sh1,000 kupata vitambulisho vya kitaifa, pesa ambazo hawana kwa sababu wengi hawana ajira.
Akiongea Jumamosi nyumbani kwake katika kijiji cha Kimunye, eneo bunge la Gichugu, Kaunti ya Kirinyaga alipotembelewa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, kiongozi huyo wa Narc Kenya alipendekeza kuwa hitaji hilo la Sh1,000 kwa vijana wanaotaka vitambulisho liondolewe.
Bi Karua aliwataka wabunge kubatilisha kanuni hiyo inayohitaji vijana kulipa ada wanapowasilisha ombi la vitambulisho vipya.
“Vijana ambao wametimu miaka 18 sharti wapewe vitambulisho bila malipo. Vijana wetu hawana ajira na wazazi wao wanazongwa na makali ya kuzorota kwa uchumi yanayoshuhudiwa kote nchini wakati huu. Kwa hivyo, vijana hawawezi kumudu kulipa Sh1,000,” akasema.
Bi Karua alidai kuwa serikali ya Rais William Ruto inawaogopa vijana wa Gen Zs waliovamia bunge Juni 25, mwaka jana kupinga Mswada wa Fedha wa 2024.
“Ruto anafahamu kuwa Gen Zs ni wengi na hivyo wanaweza kumwondoa mamlakani. Nataka kumwambia apende asipende, sharti vijana wetu wapewe vitambulisho vya kitaifa kwani hiyo ni haki yao ya kikatiba,” akaeleza.
Bi Karua, ambaye ni waziri wa zamani wa Haki na Masuala ya Kitaifa, alimtaka Rais Ruto kujitayarisha kwa ushindani mkali katika uchaguzi mkuu ujao.
“Tutamshinda Dkt Ruto waziwazi. Tutawahimiza Wakenya kuikomboa nchi hii kisiasa, kiuchumi na kijamii,” akasema
Alishutumu Rais kwa kutoheshimu Katiba ambayo aliapa kuilinda.
“Hatutamruhusu Ruto kuendesha nchi kama kwamba Katiba haipo,” akasema.
Kiongozi huyo alimlaumu kiongozi wa taifa kwa kupanga na kudhamini hoja ya kumtimua Bw Gachagua afisini mwaka jana.
“Ruto alikuwa akilalamika kuwa Uhuru Kenyatta alikuwa akimtesa. Lakini Bw Kenyatta alimruhusu Ruto kusalia afisini na hakufanikisha kutimuliwa kwake. Japo Ruto alimwondoa afisini Bw Gachagua, Wakenya wamemtawaza kuwa naibu rais wa umma,” akasema Bi Karua.
Kiongoni huwa wa Narc Kenya alimtaka Bw Gachagua kuendelea kuzungumza na Wakenya kutoka pembe zote za nchini akiendeleza ndoto zake za kisiasa.
“Ninaendeleza ndoto zangu za kuwa rais na ndugu yangu Gachagua pia anapaswa kufanya hivyo. Wakati ukitimu tutaunga mkono mgombea mmoja wa rais kupambana na Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2027,” akasema Bi Karua.
IMETAFSIRIWA NA CHARLES WASONGA