Habari

Kasipul: Aroko, Were watozwa faini ya Sh1M kwa kuchochea ghasia za uchaguzi

Na NDUBI MOTURI November 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imewatoza faini ya Sh1 milioni kila mmoja, wagombeaji wa kiti cha ubunge Kasipul, Philip Aroko na Boyd Were, baada ya kuwapata na hatia ya kuchochea na kushiriki ghasia zilizosababisha vifo vya  watu wawili, kadhaa kujeruhiwa na kusababisha uharibifu wa mali mnamo Novemba 6.

Kamati ya Utekelezaji wa Kanuni za Maadili ya Uchaguzi, inayoongozwa na Dkt Alutalala Mukhwana, ilisema wawili hao walikiuka vifungu kadhaa vya Kanuni za Uchaguzi kwa kupuuza ratiba ya kampeni iliyoratibiwa na kushindwa kuwazuia wafuasi wao.

“Ukosefu wa nidhamu wa wagombeaji hawa katika kuzingatia ratiba ndio ulisababisha vurugu, vifo na uharibifu wa mali ulioshuhudiwa Kasipul,” alisema Dkt Mukhwana Jumatano.

Uamuzi huo ulitokana na malalamishi ya pande zote mbili ambapo kila mgombea alimshtaki mwenzake kwa kuchochea makabiliano.
Aroko ambaye ni mgombea huru, alimshtaki Were na wafuasi wake kwa kushambulia msafara wake katika eneo la Opondo, akisema tukio hilo ndilo lililochochea vurugu mbaya baadaye.
Kwa upande wake, Were wa ODM alimlaumu Aroko akidai wafuasi wake walitisha wakazi katika hafla nyingine iliyohudhuriwa na Naibu Rais.

Wagombea wote walikiri kuacha kufuata njia walizopewa na IEBC, jambo ambalo kamati ilisema lilizua mazingira yaliyowezesha kukutana kwa misafara yao na kuzusha mapigano.
Afisa wa Kuratibu Uchaguzi aliambia kamati kwamba hakupokea barua ambayo Aroko alidai alituma akiomba kubadili njia; naibu wake alithibitisha kuwa barua hiyo ilitumwa usiku wa kuamkia siku ya kikao.

Ripoti za uchunguzi zilizowasilishwa mbele ya kamati zilithibitisha kuwa wawili hao waliwasilisha malalamishi kwa polisi mnamo Novemba 6 na watu wawili walifariki kutokana na ghasia hizo. Kamati pia ililaumu baadhi ya maafisa wa Serikali ya Kaunti ya Homa Bay kwa “kutumia rasilmali za umma kuendeleza vurugu za kisiasa.”

Wagombeaji hao walipatikana na hatia ya kukiuka masharti ya kuhimiza amani, kuzuia vitisho, kuwakemea wafuasi wao na kuheshimu mamlaka ya tume.

Aidha, kamati iliwapa onyo kali na kuwaagiza kufuata kikamilifu ratiba ya kampeni ya Oktoba 10. Pia waliamriwa kusaini Mkataba wa Maadili ya Kisiasa mara moja na kutoa ahadi  hadharani ya kufanya kampeni za amani.
Kamati ilionya kuwa ukiukaji mwingine wowote utaweza kusababisha kupigwa marufuku  kushiriki uchaguzi mdogo wa Novemba 27.