Kasisi John Maina alikufa kutokana na majeraha mengi ya risasi
RIPOTI ya uchunguzi wa maiti unaonyesha kuwa kasisi wa Kanisa Katoliki aliyeuawa Nyandarua John Maina alikufa kutokana na majeraha mengi ya risasi.
Kulingana na ripoti hiyo, risasi moja ilipita kichwani mwake, na kumdhuru vibaya.
Kufikia Jumatatu mchana, mwili wake ulikuwa bado umejaa damu.
Kulingana na hali ya mwili wa kasisi huyo, muuaji huyo alidhamiria kuhakikisha alikuwa amekufa wakati wanatoka katika eneo la tukio.
‘Mwili uko katika hali mbaya, ulikuwa umeharibika vibaya,’ afisa wa upelelezi ambaye alishuhudia uchunguzi huo wa maiti alisema na kuongeza kuwa ulikuwa umeanza kuoza wakati ulipotolewa.
Mwili wake ulipatikana Alhamisi, Mei 15, kando ya barabara kuu ya Nakuru-Nairobi eneo la Kikopey, takriban kilomita 50 kutoka eneo lake la kazi.
Kasisi huyo alikuwa amemkaribisha aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua katika Parokia ya Kikatoliki ya Igwamiti wiki mbili zilizopita. Bw Gachagua alikuwa mgeni mkuu wakati wa sherehe za kuadhimisha miaka 25 ya kanisa hilo.
Siku ya Jumanne, mwanapatholojia wa serikali Titus Ngulungu alifanya uchunguzi wa maiti katika hospitali ya Papa Benedict, takriban kilomita tano kutoka mji wa Nyahururu.
Hata hivyo, Dkt Ngulungu, ambaye alikuwa atoe taarifa baada ya zoezi hilo, alikataa kuzungumza na wanahabari, akinukuu maagizo makali na ripoti hiyo kutojadiliwa na Kanisa.
Uchunguzi huo wa mwili ulishuhudiwa na jamaa, Kasisi Mkuu wa Dayosisi ya Nyahururu Padre Timothy Maina na makasisi wengine 10. Ndugu na jamaa waliozungumza na Taifa Leo walieleza kutoridhishwa na jinsi kanisa lilivyoshughulikia suala hilo.
Maafisa wa upelelezi kutoka Gilgil katika Kaunti ya Nakuru ambao wanachunguza mauaji hayo pia walionekana kutokuwa na habari ya kuridhisha kuhusu kifo hicho.
Wachunguzi, hata hivyo, wanaamini kuwa Padre Maina aliuawa kwingine na mwili wake kutupwa Kikopey.
Ripoti ya mpelelezi huyo inaonyesha dakika za mwisho za kasisi huyo na jinsi aliishia Kijijini, takriban kilomita 50 kutoka Parokia ya Igwakopei.