Habari

Katibu ahepa kamati ya bunge kwenda kujivinjari Nanyuki

Na DAVID MWERE May 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KATIBU wa Vyama vya Ushirika Patrick Kilemi Jumatatu alishangaza wabunge baada ya kuamua kuenda kujivinjari kwenye warsha ya wizara eneo la Nanyuki badala ya kufika mbele ya Kamati ya Bunge la Kitaifa kutetea au kupinga mgao wa fedha kwenye idara yake katika mwaka wa kifedha wa 2025/26.

Bw Kilemi alikuwa akitakikana afike mbele ya Kamati ya Biashara, Viwanda na Vyama vya Ushirika ambayo inaongozwa na mbunge wa Ikolomani Bernard Shinali mnamo Mei 13.

Hata hivyo, hakufika kuzungumzia, kukubali au kukataa makadirio ya bajeti ya idara yake jinsi ambavyo ilichapishwa na Hazina Kuu ya Kitaifa ya Kifedha.

Wakati huo mmoja wa wasaidizi wake walimwaandikia Karani wa Bunge la Kitaifa Samuel Njoroge kuwa bosi wake hakwepo na akaomba kikao hicho kiahirishwe.

Bw Kilemi alisemekana alikuwa nje ya nchi kwa majukumu rasmi na akaomba kikao hicho wiki ya mwisho ya Mei kupitia barua iliyoandikwa na David K Obonyo na kunakiliwa kwa Waziri wa Biashara Ndogo Ndogo Wycliffe Oparanya.

Ombi hilo liliridhiwa na wabunge japo muda wa kujadili makadirio ya bajeti huwa una makataa na Bw Kilemi akatakiwa afike mbele ya kamati hiyo Mei 19 (jana).

Wabunge Maryanne Kitany ambaye ni naibu mwenyekiti wa kamati hiyo na mwenzake wa Mathare Anthony Oluoch mnamo Mei 13 walikuwa wamepinga katibu huyo kutengewa muda mwingine na hata hata kutaka kamati ipitishe mgao kwenye idara hiyo jinsi ulivyowekwa na hazina kuu.

“Ukiangalia barua hiyo si hata katibu mwenyewe ameiandika bali ni afisa wa ngazi ya chini ambaye anaomba tumtengee muda mwingine. Hili linazua swali iwapo katibu anaelewa maana ya bajeti,” akasema Bi Kitany.

“Tulimpa nafasi asikike lakini hakuja na pengine wameridhika na makadirio jinsi yalivyo,” akasema Bw Oluoch.

Licha ya msimamo wa Bi Kitany na Oluoch kamati ilimtengea Bw Kilemi jana kuwasilisha maoni yake kuhusu makadirio ya bajeti kwa idara yake lakini hakufika.

“Ndiyo katibu yuko hapa Nanyuki kwa kongamano la utendakazi na uwekaji mikakati ya idara ya serikali,” duru zikaarifu Taifa Leo.

Kwa mujibu makataa, Mei 20 (leo) ndiyo siku ya mwisho kwa kamati za bunge kukamilisha vikao kuhusu bajeti ambapo wamekuwa wakipokea maoni kutoka kwa mashirika ya serikali.

Kwa hivyo, pendekezo la katibu huyo kwamba afike mbele ya kamati wiki ya mwisho ya Mei haliwezi kutimia.