Habari

Katibu katika kikaangio kwa kuwanyima ajira vijana wa Pwani wasiozungumza Kiingereza fasaha

November 6th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

KATIBU wa Wizara ya Uchukuzi Nancy Karigithu anayesimamia Idara ya Shughuli za Meli na Ubaharia Alhamisi jioni aliwashambuliwa na Maseneta kufuatia madai kuwa aliwanyima mamia ya vijana kutoka Pwani nafasi za ajira kwa sababu wengi wao hawawezi kuzungumza Kiingereza kwa ufasaha.

Baadhi ya maseneta walitisha kuwasilisha hoja ya kujadili mienendo ya afisa huyo kwa lengo la kupendekeza afutwe kazi kwani “hawezi kuaminika na umma tena.”

“Hakuna sheria nchini Kenya inayosema kuwa lugha ya Kiingereza ni bora kulika ile ya Kiswahili au Kiswahili ni bora kuliko Kiingereza,” akafoka Seneta wa Kilifi Stewart Madzayo.

Bi Karigithu imeripotiwa alidai kuwa vijana kutoka Pwani hufeli kupata ajira katika kampuni za meli za kimataifa kwa kukosa umilisi wa lugha ya Kiingereza.

Katibu huyo alisema tangu mwaka 2019 ameshiriki shughuli ya kuhoji na kuajiri wahudumu wa meli Mombasa kwa niaba ya mashirika ya meli ya kigeni lakini alishtuka kubaini kuwa baadhi ya vijana waliokuwa wakisaka nafasi hizo za ajira walishindwa kujieleza kwa lugha ya Kiingereza.

“Hili ni suala muhimu zaidi; sharti vijana wanoe uwezo wao wa kuzungumza Kizungu. Lugha za Sheng na zile ambazo hutumiwa katika mitandao ya kijamii kama vile WhatsApp hazina umuhimu wowote wakati wa kusaka ajira. Kiingereza ndiyo lugha inayohitajika katika sekta ya ubaharia,” Bi Karigithu aliripotiwa akisema.

Seneta Madzayo ambaye hupenda kuchangia mijadala bungeni kwa lugha ya Kiswahili, alitaja madai ya Katibu huyo wa Wizara kuwa ni matusi sio tu kwa vijana, lakini kwa jamii zote za Pwani.

“Kamati ya Seneti kuhusu Uchukuzi inafaa kuamwamuru Katibu huyo afike mbele yake ili aeleze ni sheria gani ya Kenya inayosema kuwa sharti mtu awe anaweza kuongea Kiingereza ndiposa apate kazi za serikali,” Seneta huyo akapendekeza, kauli iliyoungwa mkono na Seneta wa Lamu Anwar Loitiptip.

“Baada ya kumhoji Bi Karigithu, sharti kamati hiyo iandae ripoti na kuiwasilisha mbele ya kikao cha maseneta wote,” akasema Bw Loitipitip ambaye ni Seneta wa chama tawala, Jubilee.

Seneta wa Mombasa Mohamed Faki alisema Katibu huyo inafaa apigwe kalamu kwa kusaliti imani ya umma kwa afisi anayoshikilia.

Naye Seneta wa Taita Taveta Johannes Mwaruma alisema kuwabagua vijana wa Pwani katika ajira ni sehemu ya mpango wa “kimakusudi” wa kuendeleza umaskini katika eneo zima.

“Ikiwa wakazi wa Pwani hawaajiriwi au kupewa nafasi za kujiendeleza, hii ina maana kuwa umaskini utaendelea kusakama watu wetu,” akasema Bw Mwaruma.

Akaongeza: “Kitendo hicho cha Karigithu ni ubaguzi uliokithiri mipaka.”

Alisema ikiwa Wakenya watakaoajiriwa katika sekta hiyo ya uchukuzi wa meli na ubaharia hawafahamu Kiingereza vizuri wanaweza kufundishwa.

“Huyu Katibu wa Wizara anafaa kushtakiwa kwa Afisi ya Kupokea Malalamishi kutoka kwa umma (Ombudsman). Bi Karigithu amehujumu haki za watu wa eneo la Pwani,” akasikitika.