Habari

Kawira alaumu sheria kwa kutimuliwa kwake, asema inakiuka katiba

Na CHARLES WANYORO, BENSON MATHEKA August 17th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

GAVANA wa Meru Kawira Mwangaza anaitaka Mahakama Kuu kutangaza sheria inayowaruhusu madiwani kufufua hoja ya kumuondoa Gavana baada ya miezi mitatu kuwa kinyume cha katiba.

Gavana huyo anataka mahakama ya Kikatiba na Haki za Kibinadamu iamue kwamba kifungu cha 33 (8) cha Sheria ya Serikali ya Kaunti kinakiuka haki za magavana waliochaguliwa na wapiga kura.

Sehemu hiyo inawaruhusu Wawakilishi wa Wadi kuwasilisha tena hoja ya kuondoa gavana, miezi mitatu baada ya  Seneti kukataa kuidhinisha kuondolewa kwa gavana.

“Ikiwa kura katika Seneti itakosa kusababisha kuondolewa kwa gavana, Spika wa Seneti atamjulisha spika wa bunge la kaunti husika ipasavyo na hoja ya bunge ya kumuondoa gavana huyo kwa madai sawa inaweza tu kuwasilishwa tena kwa Seneti baada ya muda wa miezi mitatu kuanzia tarehe ya kupiga kura kama hiyo,” inasema sheria ya serikali ya kaunti.

Bi Mwangaza ambaye anapigana katika seneti baada ya kuondolewa kwa mara ya tatu katika muda wa miaka miwili, anasema sheria hiyo inaweka magavana katika hatari maradufu ambapo mtu anaweza kulaumiwa mara kwa mara kwa kosa sawa kila baada ya miezi mitatu.

Anamuomba Jaji Edward Muriithi kuamua bunge  la kaunti lilitumia mamlaka yake kwa njia isiyo halali, kupita kiasi na vibaya.

Kupitia kwa mawakili Elias Mutuma na Ashaba Mark, gavana huyo anasema hilo ni pengo la kisheria ambalo linafanya madiwani  kuzoea kumtimua gavana aliyechaguliwa na watu wengi.

“Sio haki baada ya kuchaguliwa na watu wengi kama gavana,  unakabiliana na hoja za kukutimua kila baada ya miezi mitatu,” alisema Bw Ashaba.

Bi Mwangaza anasema haki zake  anazohakikishiwa kupitia Kifungu 50(1) cha Katiba ya Kenya zitakiukwa, hasa haki ya kusikilizwa, akisema kuwa bunge la kaunti lilikuwa likimbagua.

Kwa hivyo anaitaka mahakama kumuokoa na hatari maradufu ya mchakato anaodai kuwa umechochewa kisiasa.

Hata hivyo,  madiwani kupitia wakili Ndegwa Njiru wanasisitiza kuwa Mahakama Kuu haina mamlaka ya kusikiliza ombi la Bi Mwangaza na kumtaka aliondoe.

“Mahakama hii Tukufu sio jukwaa lililowekwa na Katiba kuhoji uhalali, dosari, ukweli au uwongo wa tuhuma zilizofafanuliwa katika hoja ya kumtimua,” alisema.

Jaji Muriithi alitoa uamuzi  Septemba 5, 2024.