Habari

Kawira apata chama kipya na kuteua mumewe, mwanawe na dadake kwenye nyadhifa

Na DAVID MUCHUI July 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA Gavana wa Meru, Kawira Mwangaza, wikendi alizindua chama chake kipya, akiapa kuwa atalipiza kisasi cha kisiasa kwa viongozi waliochangia kuondolewa kwake madarakani.

Bi Mwangaza na familia yake hivi majuzi walichukua usukani wa chama cha UMP kinachohusishwa na Gavana wa zamani wa Embu, Martin Wambora.

Akiwahutubia wafuasi wake kwenye makazi ya Ntumburi wakati wa uzinduzi wa chama hicho, Bi Mwangaza alisema kuwa moto wake wa kisiasa ndio umeanza kuwaka baada ya kuondolewa afisini.

Hata hivyo, kiongozi huyo amewashangaza wengi baada ya kuweka wanafamilia wake washikilie nyadhifa mbalimbali chamani.

Bi Mwangaza atakuwa kiongozi wa chama, mwanawe Victor Koome awe naibu kiongozi wa chama kisha mumewe Murega Baichu atahudumu kama katibu mkuu.

Dadake Miriam Karwirwa atakuwa mwenyekiti huku aliyekuwa mkuu wa wafanyakazi wa kaunti kwenye utawala wake Harrison Gatobu akiwa mkurugenzi wa chama.

Notisi ya gazeti iliyochapishwa Julai 4 na aliyekuwa Msajili wa Vyama vya Kisiasa Ann Nderitu ilionyesha kuwa makao makuu ya UMP yamehamishwa kutoka Embu hadi nyumbani kwa Bi Mwangaza katika kijiji cha Kamuketha.

Bi Mwangaza anafahamika kuwachangamisha raia na kujizolea ufuasi mkubwa kupitia mpango wake wa kushiriki miradi ya kuinua jamii maarufu kama ‘Okolea’.

Sasa anajiunga na viongozi wengine kutoka kaunti hiyo ambao wanamiliki vyama vya kisiasa. Viongozi hao ni Kiraitu Murungi (DEP), Peter Munya (PNU) na Mpuru Aburi (NOPEU).

Bi Mwangaza alichaguliwa kama mgombeaji huru mnamo 2022 na sasa anasema kuanzisha chama kipya kumechangiwa na mafunzo aliyoyapata kutokana na kutimuliwa kwake na madiwani bila chama.

Aliwalaumu mahasimu wake wa kisiasa Mabw Murungi na Munya kwa kuwatumia madiwani ili kumbandua madarakani.

“Kama singeondolewa, singebuni UMP. Wanasiasa wakubwa ambao walipoteza kura 2022 waliungana kisha kuning’oa. Sasa nina chama kama wao na nitashughulikia dhuluma zilizochangia kuondolewa kwangu,” akasema Bi Mwangaza.

Alijipiga kifua kuwa chama hicho kitashinda viti vyote Meru ambako viongozi wengi waliochaguliwa wamekuwa wakimpiga vita.

“Tutawania viti vyote hasa vya wale walionisaliti. Tutahakikisha kuwa wote wanashindwa kura ikifika,” akaongeza.

Chama kipya cha Bi Mwangaza kinatarajiwa kupambana na kile cha UDA cha Rais William Ruto na pia cha DCP cha aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua ambacho kinaendelea kupata ufuasi katika kaunti hiyo.

Katibu Mkuu wa DEP, Mugambi Imanyara, mwandani wa Bi Mwangaza, alisema chama hicho nacho kitawapiga msasa wawaniaji wote na wale waliochangia kutimuliwa kwa Bi Mwangaza hawatapewa tikiti.

“Kama ulishiriki katika kutimuliwa kwa Bi Mwangaza basi chuma chako ki motoni kwa sababu watu watazungumza debeni,” akasema Bw Mugambi.

Kupima nguvu zake, Bi Mwangaza alisema UPM itakuwa na mwaniaji katika uchaguzi mdogo wa Mbeere Kaskazini, Kaunti ya Embu.