‘Kazi majuu’ yaacha vijana kwenye mataa
VIJANA waliojisajili katika mpango wa serikali wa ‘Kazi Majuu’ sasa wahofia kupoteza mali zao walizoweka kama dhamana ya mkopo wa serikali kughararamia safari zao.
Vijana hao kutoka maeneo ya Pwani na Nairobi sasa wanataka serikali kuingilia kati kuwatatulia kizungumkuti hicho.
Miezi kadhaa baada ya kuomba ajira za ughaibuni chini ya mpango huo na kukopa kutoka kwa hazina ya vijana inayosimamiwa na serikali, zaidi ya vijana 500 sasa wamesalia bila ajira huku wengine wakikatwa mishahara yao michache kulipia deni kabla ya kusafiri.
Kulingana na waathiriwa, serikali iliwapa nafasi ya kukopa Sh200,000 kutoka kwa hazina ya vijana ili kugharamia safari za wale ambao wanatoka katika familia zisizojiweza. Walielezwa kuwa wanapaswa kuanza kulipa baada ya miezi mitatu.
‘Baada ya kufanya majaribio ya kazi tuliambiwa tutasafiri ndani ya muda wa miezi mitatu. Hata hivyo miezi saba baadae bado hatujasafiri na hatujui hatima yetu,’ akasema Bi Saada Hafidh, mmoja wa vijana.
Alisema baadhi ya vijana wenzao wameanza kukatwa deni hilo kwa mishahara yao, hali inayowatia hofu wale ambao hawana ajira.
‘Kuna baadhi wameanza kukatwa mshahara ili kulipa deni, sisi ambao hatuna ajiri itakuwaje, hatutaki kupoteza mali zetu,’ akasema Bi Saada.
Bi Diana Tunga, kijana mwingine anayefanya kazi kama mhudumu katika klabu mjini Kilifi, alisema mshahara wake umeanza kukatwa japo bado hajasafiri.
‘Makubaliano ilikuwa tutakatwa Sh33,334 kila mwezi baada ya kuanza kazi nje lakini nashangaa mshahara wangu wa Sh25,000 umekatwa Sh18,000 kulipa deni,’ akasema Bi Tunga akiongezea kuwa hatua hiyo imemfanya kushindwa kukidhi baadhi ya mahitaji yake.
Alisema japo vijana wenzake waliacha kazi kujiandaa na safari, yeye aliendelea na kazi akisubiri hadi pale visa yake itakapopatikana.
Wengine waliamua kuachia kazi zao hapa nchini kujiandaa kwa nafasi ambazo hazikuwapo, na kuishia wakiwa kwenye msongo wa kifedha na kitaaluma.
Bi Tunga alisema juhudi zake za kutafuta usaidizi kutoka kwa afisi ya hazina ya vijana hazijafua dafu.
Mpango wa Kazi Majuu, ulioanzishwa Juni 2023, ulilenga kufungua ajira za kimataifa kwa vijana wa Kenya.
Wengi walikopa kutoka Youth Fund kugharamia gharama za safari na awali, wakidhani ni uwekezaji wa maisha yao.
“Nilikopa kwa sababu niliamini mpango huu. Sasa nahisi nimekwama. Sina kazi hapa, sina kazi nje ya nchi,” alisema Bi Hafidh.
Mwakilishi wa shirika la Zawadi, ambalo ni mojawapo ya mashirika yaliyokuwa yakitafutia vijana ajira ughaibuni, alithibitisha kuwa wanashikilia pasipoti za vijana zaidi ya 100 lakini haijulikani watasafiri lini.
“Tunaendelea kushirikiana na waajiri wa nje, lakini hatuwezi kuthibitisha lini watasafiri. Tunaomba uvumilivu,” aliambia Taifa Leo kwa njia ya simu.
Waliotuma maombi wanaiomba serikali kuingilia kati mara moja, kuacha punguzo la mishahara na kurudisha pasipoti zao.
Aidha waliiomba serikali kuhakikisha vijana waliosoma wanapata kazi za afisini kama walivyoahidi wakati wa maombi.
‘Nilikuwa nimetafuta kazi ya ofisi lakini sasa nalazimishwa kukubali kazi ya kufanya usafi, ambayo mshahara wake ni mdogo na masaa ya kazi ni mengi ukilinganisha na kazi niliyokuwa nimefanyiwa majaribio,’ akasema Bi Hafidh.
Mwakilishi wa Hazina ya Vijana aliyeomba kutotajwa, aliwasihi vijana wanaopitia changamoto hizo wawasilishe malalamishi rasmi ili wasaidiwe.
Kulingana naye, iwapo kuna mishahara inayokatwa kulipia deni, suala hilo linaweza kusitishwa kupitia kwa mfumo rasmi.
Alisema kuna vijana kadha ambao walishawezeshwa kuongeza muda ambao utachukuliwa kabla waanze kudaiwa fedha walizokopa.