MABADILIKO katika kuhesabu alama za wastani kwa wanafunzi katika mtihani wa (KCSE yamesababisha ongezeko la wanafunzi waliopata alama bora, jambo linalofungua fursa zaidi za elimu ya juu na mafunzo ya kitaaluma.

Kulingana na Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Kitaifa (KNEC), Dkt David Njeng’ere, matokeo yaliyotolewa jana yamefanya Kenya kukaribia nchi ambazo wanafunzi wanaostahili kujiunga na vyuo vikuu kuwiana na idadi ya kawaida ya watu ambako hakuna majanga kama vita, njaa au janga la afya.

Alieleza kuwa mafanikio haya yametokana na mabadiliko katika jinsi ya kuhesabu alama za wastani yaliyoanza mwaka 2023.

Kwenye kigezo kipya, baraza huchambua wanafunzi kwa kutumia masomo saba badala ya masomo nane ya awali.

Haya ni Hisabati, lugha bora zaidi kati ya Kiingereza, Kiswahili au Lugha ya Ishara ya Kenya, pamoja na masomo matano bora zaidi ya mtahiniwa.

Tangu wakati huo, idadi ya wanafunzi wanaofunzu kujiunga na vyuo vikuu imekuwa ikiongezeka. Matokeo ya KCSE 2025 yameorodhesha idadi kubwa zaidi ya wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu tangu marekebisho makali ya mitihani ya kitaifa yalipoanzishwa mwaka 2016.

Wanafunzi 270,715 kati ya 993,226 waliofanya mtihani walipata kiwango cha C+ na juu, jambo linalowastahikishia kujiunga na vyuo vikuu.

Kwa asilimia 27.18, kiwango cha wanaojiunga na vyuo vikuu kinazidi asilimia 25.53 ya mwaka 2024, asilimia 22.3 mwaka 2023, asilimia 19.03 mwaka 2022, na asilimia 11.3 mwaka 2017.

“Kwa muda mrefu, tumekuwa chini ya asilimia 20. Kwa mfumo wa elimu kama huu, ina maana hauwezi kupata wafanyakazi wanaofunzwa kwenye vyuo ili kusaidia ukuaji wa uchumi,” alisema Dkt Njeng’ere.

Alibainisha kuwa ongezeko la asilimia ya wanafunzi wanaofunzu kujiunga na vyuo vikuu linaashiria kuwa nchi iko kwenye mwelekeo sahihi, ikifuata mifano ya nchi kama Zambia (asilimia 50) na Korea Kusini (asilimia 70).

Ingawa kimataifa hakuna kiwango kimoja kilichowekwa, miongozo ya sera za elimu na ripoti za Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) hutoa viwango vya jumla vya kati ya asilimia 30 hadi 40.