Habari

KCSE 2025: Watahiniwa 1,180 kukosa matokeo yao

Na BENSON MATHEKA January 10th, 2026 Kusoma ni dakika: 1

WIZARA ya Elimu imefuta matokeo ya watahiniwa 1,180 wa Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) 2025 baada ya kubainika walihusika katika vitendo vya udanganyifu wa mitihani.

Waziri wa Elimu, Bw Julius Ogamba, alisema hatua hiyo ilichukuliwa kufuatia kukamilika kwa uchunguzi kuhusu visa vya ukiukaji wa kanuni za mitihani vilivyoripotiwa wakati wa kufanya mtihani mwaka jana.

Akizungumza wakati wa kutangaza rasmi matokeo ya KCSE, Bw Ogamba alisisitiza kuwa serikali haitavumilia vitendo vyovyote vinavyodhoofisha uadilifu wa mitihani ya kitaifa.

“Ningependa kusisitiza tena msimamo wetu kuhusu uadilifu wa mitihani. Mnamo Novemba mwaka jana, tulieleza kuwa kulikuwa na visa vilivyoripotiwa ambavyo vilikuwa vinafanyiwa uchunguzi, na kwamba hatua zingechukuliwa baada ya uchunguzi kukamilika,” alisema waziri huyo.

Aliongeza kuwa baada ya mtihani kukamilika, ilibainika kuwa watahiniwa hao 1,180 walihusika moja kwa moja au kwa njia zisizo halali katika udanganyifu wa mitihani.

“Hivyo basi, kwa kuzingatia sheria na kanuni husika, matokeo yao ya mtihani yamefutiliwa mbali,” alisema jijini Eldoret jana.