KCSE yaanza onyo kali likitolewa kuhusu udanganyifu
MTIHANI wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) wa mwaka 2025 ulianza jana kote nchini baada ya Mtihani wa Tathmini ya Elimu ya Shule za Msingi za Junior (KJSEA) kukamilika.
Katika Kanda ya South Rift, watahiniwa katika Shule ya Upili ya Wavulana ya Litein, Kaunti ya Kericho, walirejea masomoni na kuungana na maelfu ya wengine kuanza mitihani baada ya mahakama kuruhusu shule hiyo kufunguliwa tena.
Watahiniwa 429 walikuwa wamerejeshwa nyumbani kufuatia ghasia zilizoharibu mali ya thamani ya Sh100 milioni ambapo mahakama ilipunguza ada ya fidia kutoka Sh49,699 hadi Sh25,000 kwa mwanafunzi ambayo italipwa kwa awamu.
Katika Kaunti ya Samburu, Kamishina wa Kaunti John Cheruiyot aliwahakikishia wanafunzi na walimu usalama wa kutosha katika maeneo yanayokumbwa na ujambazi.
“Helikopta ipo tayari kusafirisha vifaa vya mitihani katika vituo rasmi endapo kutahitajika. Tuko makini kuhakikisha mitihani inaendelea bila tatizo,” akasema. Taifa Leo ilishuhudia shule nyingi zikianza mitihani kwa wakati.
Katika Kaunti ya Nakuru, Kamishina Loyford Kibaara alisema usalama umeimarishwa katika vituo vyote na akaonya dhidi ya udanganyifu wa mitihani. Afisa wa utawala wa kaunti ndogo ya Nakuru East, Simiyu Were, alisimamia ufunguzi wa makontena ya mitihani na kuwataka wazazi na wananchi kwa ujumla kudumisha utulivu.
Kikosi cha pamoja cha maafisa wa elimu na polisi kilihakikisha shughuli zinaendelea vizuri.
Ukanda wa Mlima Kenya ulishuhudia mtahiniwa mmoja katika Kaunti ya Laikipia akifanya mtihani wake katika Hospitali ya Rufaa ya Nanyuki Level Five baada ya kujifungua. Mkurugenzi wa Elimu wa Kaunti, Bridget Wambua, alisema maandalizi yalifanywa kuhakikisha anafanya mitihani kwa urahisi.
Licha ya mvua kubwa, watahiniwa 11,162 waliojiandikisha katika vituo 143 walianza mitihani bila usumbufu mkubwa.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Baraza la Kitaifa la Mitihani (KNEC), Dkt. David Njeng’ere, alisambaza kufuli za kidijitali zilizounganishwa moja kwa moja na makao makuu ya KNEC ili kuimarisha uadilifu wa mitihani.
Wakati huo huo, jumla ya watahiniwa 163,925 wanafanya mitihani katika vituo 2,218 katika Kanda ya Mashariki.
Mkurugenzi wa Elimu wa eneo hilo, Friendrick Muturi, alisema shughuli hiyo ilianza vizuri chini ya ulinzi mkali, huku akiahidi kuhakikisha mitihani inafanyika kwa uwazi na uaminifu.
Hakuna visa vilishuhudiwa Kaskazini Mashariki mwa Kenya, huku Mkurugenzi wa Elimu wa Kanda, Adan Roble, akisema mitihani ilianza vyema. Helikopta zilitumika kusambaza vifaa vya mitihani katika maeneo yaliyoathirika na mafuriko na ukosefu wa usalama kama vile Balambala, Garissa, na Wajir Kaskazini.
Kanda hiyo ina jumla ya watahiniwa 27,018 kutoka vituo 239 wakiwemo wavulana 16,465 na wasichana 10,552.
Katika Bonde la Ufa, mwanafunzi mmoja aliyejeruhiwa wakati wa maporomoko ya ardhi katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet hapo Novemba 1 anafanya mtihani wake katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi.
Akizungumza akiwa Kaunti ya Kwale, Waziri wa Elimu Julius Ogamba alithibitisha kuwa helikopta zinatumika kusafirisha vifaa vya mitihani katika maeneo yaliyoathiriwa na mvua kama Trans Nzoia. Alisisitiza umuhimu wa usahihishaji wa haki kupitia mfumo wa kuficha majina ya watahiniwa na akaonya dhidi ya udanganyifu wa mitihani, akisema yeyote atakayekamatwa akihusika atachukuliwa hatua kali za kisheria na kufutwa kazi.
Bw Ogamba pia alirejelea dhamira ya serikali kuhakikisha asilimia 100 ya wanafunzi wanaendelea na masomo, akibainisha kuwa nafasi zipo katika vyuo vikuu na vyuo vya kiufundi (TVET). Alisema idadi kubwa ya watahiniwa mwaka huu imetokana na kundi la Wanafunzi wa gredi ya tisa, wakiwa zaidi ya 1,000,030.
Katika Kaunti ya Tana River, Naibu Kamishina wa Kaunti Andrew Mutua alisema makontena yenye kufuli za kisasa yamewekwa katika maeneo yanayokumbwa na mafuriko ili kulinda vifaa vya mitihani.
Mkurugenzi wa Elimu wa Kaunti ya Lamu, Zachary Mutuiri naye alionyesha matumaini ya matokeo bora kutokana na utulivu na hali nzuri ya mazingira.
Katika Kaunti ya Mombasa, Mkurugenzi wa Elimu Musibo Kitui aliwataka walimu na wasimamizi kudumisha weledi na kukabidhi simu zao kulingana na kanuni za mitihani.
Katika Kaunti ya Taita Taveta, afisa wa KNEC Pauline Waweru alisimamia ufunguzi wa makontena ya mitihani mjini Voi, huku Mkurugenzi wa Elimu wa Kaunti, Khalif Hirey akithibitisha kuwa zoezi hilo lilianza kwa utulivu.