KEN OKOTH: Rais Kenyatta, viongozi wengine watuma salamu za pole
Na CHARLES WASONGA
RAIS Uhuru Kenyatta, viongozi na Wakenya kutoka tabaka mbalimbali Ijumaa wametuma salamu za pole kwa familia, jamaa na marafiki wa mbunge wa Kibra, Ken Okoth ambaye amefariki saa kumi jioni katika Nairobi Hospital.
Kiongozi wa nchi amemtaja Okoth kama kiongozi aliyeonyesha mfano bora wa uadilifu kiasi kwamba alizingatia sana kutumikia taifa na hasa wakazi wa eneobunge la Kibra.
“Nimehuzunika kupokea habari za kifo cha Kenneth Okoth, mbunge wa Kibra. Naomba Mungu aipe familia yake, wandani, jamaa, wakazi wa eneobunge lake na taifa kwa jumla nguvu wakati huu mgumu,” amesema kiongozi wa nchi.
Naye kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga amemtaja marehemu kama kiongozi aliyepigana na saratani ya utumbo kwa ujasiri mkubwa.
“Ninasikitika sana kupata tanzia kwamba Ken Okoth amefariki. Kwa kweli apambana na saratani kwa njia ya kipekee ya kuonyesha ukakamavu ambapo hali hii haikuondoa dhamana aliyokuwa nayo ya kuwawakilisha wakazi wa Kibra,” ameandika Raila kwenye ujumbe wa ukurasa wa akaunti yake ya Twitter.
Naye spika wa bunge la kitaifa, Justin Muturi, ameelezea kwamba kwa takribani miaka saba sasa amemjua kama kiongozi aliyejitolea kubadilisha kwa kuboresha maisha ya watu wa Kibra.
“Habari za kifo chake zinakuja mnamo wakati ambapo tulikuwa na matumaini makubwa kwamba alikuwa ameanza kupata nafuu,” amesema Muturi.
Kulingana na Imra Okoth ambaye ni meneja wa afisi ya eneobunge la Kibra, marehemu Okoth alifariki baada kuomba mitambo ya kusitiri maisha yake yazimwe.
“Mheshimiwa aliletwa katika Hospitali ya Nairobi mwendo wa kumi na moja jioni jana Alhamisi. Hali yake ilipoendelea kuwa mbaya alihamishwa hadi katika kitengo cha wagonjwa mahututi ambako alifariki baada ya saa moja iliyopita,” Bw Okoth akawaambia wanahabari nje ya hospitali hiyo.
Marehemu Okoth aliingia bungeni kwa mara ya kwanza mnamo 2013 baada ya eneobunge la Kibra kugawanywa kutoka kwa eneobunge la Langata.
Eneo hilo zamani lilikuwa likiwakilishwa na kiongozi wa ODM Raila Odinga tangu 1992.