Habari

Kenei: Familia yataka ukweli, Ruto akitetewa

March 7th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

PETER MBURU, MERCY KOSKEI na SAMUEL BAYA

MATAMSHI na maandishi kutoka kwa Naibu Rais William Ruto pamoja na wafuasi wake yanayoashiria kunyooshea baadhi ya asasi kidole cha lawama kuhusu mauaji ya aliyekuwa mkuu wa usalama katika afisi yake Kipyegon Kenei yaliendelea Ijumaa huku familia ya afisa huyo ikitoa wito mawasiliano yanayodaiwa kufutwa katika simu ya Bw Kenei yawekwe wazi.

Wakiongozwa na Dkt Ruto mwenyewe, viongozi hao walishambulia Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) kuwa ndiyo inavuruga uchunguzi, na pia wakaitaka kampuni ya mawasiliano ya Safaricom kufafanua kuhusu rekodi za mawasiliano ya simu ya marehemu.

“Ukweli sharti upatikane kuhusu kwa nini, vipi na nani alimuua Bw Kenei. Familia yake, afisi ya Naibu Rais na Wakenya wanataka ukweli na haki na washukiwa kuadhibiwa. Vitimbi, uvurugaji na kuficha ukweli vinachangia kuficha uhalifu usibainike,” Dkt Ruto akasema kupitia akaunti ya mtandao wa Twitter.

Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen naye pia alikashifu DCI kwa madai ya kuficha ukweli kuhusu mauaji hayo.

“Kwa nini DCI anaficha matokeo ya uchunguzi wa kisayansi kutoka kwa maabara ya serikali? Anaficha nini? Kulikuwa na jaribio la kuhamisha msimamizi wa idara ya silaha katika DCI? Kwa nini? Wakenya wanataka kujua ukweli,” Bw Murkomen akasema.

Viongozi wengine wakihusisha seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot, mfanyakazi katika afisi ya Dkt Ruto Dennis Itumbi na mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung’wa pia ni baadhi ya waliozidisha kelele kupitia mitandao ya kijamii, zote zikiwa kulaumu DCI na kuitaka Safaricom kueleza ni mfanyakazi yupi alifuta rekodi za mawasiliano katika simu ya Bw Kenei.

Wakati wao wakiendelea na kelele za kisiasa na kutupa lawama huku wakitetea afisi ya Dkt Ruto, familia ya marehemu ilitoa wito kuwa mawasiliano ya data yaliyofutwa katika simu ya mwanao yawekwe wazi kwa umma.

Bw Kenei alipatikana akiwa ameuawa wiki mbili zilizopita katika nyumba alimokuwa akiishi, katika mtaa wa Imara Daima, Nairobi.

Mnamo Ijumaa, babake Bw Kenei, John Chesang alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutazama mwili wa mwanawe hapo jana alisema kuwa familia inasubiri habari hizo kuwekwa wazi ili zisaidie kutoa ukweli.

“Sisi kama familia tulifurahia wakati DCI walitangaza kuwa aliuawa. Hata hivyo, tunaomba serikali iweze kuweka matokeo hayo wazi kama walivyoweka yaliyotokea kwenye Afisi ya Naibu Rais,” Bw Chesang akasema.

Alisema kuwa ingawa familia ilipokea matokeo ya upasuaji, kwao haikuwa thibitisho tosha kuhusiana na mauaji ya mwanao.

“Upasuaji wa maiti hauwezi kuwanasa wauawaji. Tunafurahi kwamba mkurugenzi wa DCI alionyesha matukio siku ya alhamisi lakini sasa tunataka mawasiliano ya simu yake pia yawekwe wazi,” akasema Bw Chesang.

Aliongeza kuwa familia ina matumaini kuwa wale waliomuua watatiwa nguvuni kabla ya Kenei kuzikwa Jumamosi.

Wakati wa kutazama maiti ya Bw Kenei katika hifadhi ya maiti ya Umash mnamo Ijumaa, familia, marafiki na jamaa za mwendazake Kenei walijawa na majonzi, wakilia kwa uchungu, naye mjane wa Bw Kenei, Judy Kipsoi kulemewa.

“Nitawaeleza vipi wana wetu pindi watakapokua wakubwa kuwa baba yao aliluawa akiwa kazini. Nina huzuni kubwa sana kama mama ila tunamwachia mwenyezi Mungu yote yaliyotendeka,” akasema.