Habari

Kenya iko tayari kwa uwekezaji wa Amerika, Rais Kenyatta afahamisha

September 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na PSCU

RAIS Uhuru Kenyatta amewataka wawekezaji wa Amerika kuifanya Kenya kuwa chaguo lao barani Afrika.

Rais alisema Nguzo Nne za Ajenda Kuu ya Maendeleo ya Serikali yake, hususan uzalishaji ambapo Serikali inapanga kuinua mchango wa sekta hiyo kwenye uchumi kutoka asilimia 8.4 ya sasa ya Pato la Kitaifa hadi asilimia 15 ifikapo mwaka 2022, inatoa nafasi nyingi kwa kampuni za Kimarekani.

“Sekta ya uzalishaji inatoa nafasi kubwa kwa waekezaji wa humu nchini na wale wa kigeni katika nyanja kama vile utayarishaji wa mazao ya kilimo kwa kuongeza thamani katika sekta kuu ikiwemo sekta ya ushonaji nguo na ngozi, uchumi wa baharini, ujenzi, vyuma, mafuta na gesi,” kasema Rais.

Rais Kenyatta aliyehutubia kongamano la sekta ya kibinafsi lililoandaliwa na Shirika la Biashara nchini Marekani na kuhudhuriwa na maafisa wakuu wa kampuni kubwa za kimataifa kutoka Marekani alisema inatafuta ushirikiano wa kudumu wa kibiashara na mashirika ya Marekani.

“Tunapoimarisha uhusiano kati ya Kenya na Marekani, ni ushirikiano na mashirika kama yale mnayowakilisha, ndiyo huongoza na kudumisha uhusiano,” Rais kawaambia maafisa hao wakuu wakiongozwa na Scott Eisner, ambaye ni Rais wa Kituo cha Biashara kati ya Marekani na Afrika ambaye vilevile ni Naibu Mkuu wa Rais Shirika la Biashara nchini Amerika.

Kando na uzalishaji, Rais alisema kujitosheleza kwa chakula na lishe bora, makaazi nafuu na Afya Bora kwa Wote ni sekta zingine ambazo zina uwezo mkubwa wa uekezaji.

Rais Kenyatta alisema lengo la Serikali yake la kujenga nyumba 500,000 za gharama nafuu lingalipo na akazirai kampuni za Marekani kutenga rasilimali kwa mpango huo.

“Zaidi ya nusu ya ufadhili wa mpango huu wa makazi utatokana na rasilimali za sekta binafsi. Vilevile tutatarajia kuwekeza katika vifaa mbadala vya ujenzi na teknolojia,” akasema Rais Kenyatta.

Kuhusu mpango wa Afya Bora kwa Wote, Rais alitoa wito wa ushirikiano; hasa katika usambazaji wa vifaa maalumu vya afya, kuanzishwa kwa kampuni za kutengeneza dawa, kuboresha na kusimamia vifaa vya afya na utekelezaji wa chaguo mbalimbali za ufadhili wa afya kwa njia ya ubunifu.

Mwaliko

Mbali na nyanja hizo nne kuu, Rais alitoa mwaliko kwa wawekezaji kutafakari kuhusu nafasi katika sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, miundomsingi, utalii na uchumi wa rasilimali za baharini.

Alishauri jumuiya ya wafanyabiashara wa Amerika kulenga zaidi sekta ya fedha nchini Kenya ambapo taifa hili linatambuliwa ulimwenguni kutokana na suluhisho la kifedha kupitia simu ya rununu.

“Mfumo wa fedha kwa njia ya kidijitali umeimarika na kutoa huduma za ziada za kisasa ikiwemo bima, kulipia bidhaa na huduma, malipo ya uzeeni na kutolewa kwa bondi za kifedha za serikali katika viwango vidogovidogo na nafuu kwa umma.

“Uwekezaji mkubwa na nafasi za ukuaji zinaendelea kuwepo kwenye sekta hii thabiti inayoendelea kuimarika,” akasema kiongozi wa nchi.

Rais pia alisema anaridhika na ongezeko la idadi ya kampuni za Kimarekani ambazo zinaanzisha biashara nchini Kenya katika miaka ya hivi maajuzi.

“Nafurahi kutambua kwamba tangu kukutana kwangu na jamii ya wafanyabiashara wakati kama huu mwaka 2018 baadhi ya kampuni za Amerika zimengia kwenye soko la Kenya na kufungua afisi na matawi,” akasema.

Kiongozi wa nchi aliyeongoza ujumbe wa ngazi za juu akiwemo Gavana wa Kaunti ya Nakuru Lee Kinyanjui, alikaribisha wawekezaji na akawahakikishia kuungwa mkono kikamilifu na Serikali.

“Tunatarajia sio tu kuhakikisha kwamba biashara zenu zinanawiri, lakini pia nyinyi kuchangia maendeleo ya Kenya kwa kubuni nafasi za kazi, pamoja na kueneza rasilimali na teknolojia,” Rais Kenyatta akawahakikishia viongozi hao wa kampuni za Amerika.

Alisema uchumi wa Kenya ni thabiti na kwamba Serikali yake inaendelea kutekeleza hatua kwa hatua mabadiliko ya sera, soko na miundomsingi ambayo itahakikisha kunawiri kwa mazigira mwafaka ya biashara.

“Kwa kampuni ambazo hazijawekeza nchini Kenya, nawashauri muwasiliane na wenzenu ambao tayari wanafanya kazi nchini Kenya.

“Watawapa hakikisho kwamba nchini Kenya, utapata uchumi thabiti unaokua kwa asilimia 6 kila mwaka, nguvukazi yenye elimu bora na maarifa ya ujasiriamali, mazingira mwafaka ya ya kufanyia biashara pamoja na mfumo stadi wa uchukuzi na muundomsingi wa Teknolojia ya Haabri na Mawasilino,” kasema Rais.

Kiongozi wa Taifa alitaja reli ya kisasa ya SGR kutoka Mombasa-Nairobi-Naivasha na bandari mpya ya Lamu kuwa sehemu ya miradi mikubwa ya Miundomsingi iliyotekelezwa na Serikali yake kuimarisha mazingira ya kibiashara katika taifa hili la Afrika Mashariki.

Mapema, Rais Kenyatta alifanya mashauri mbalimbali ya pande mbili na Rais wa Ureno Marcelo Rebelo de Souza na Waziri Mkuu wa Denmark Mette Frederiksen pembezoni mwa Kongamano la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York.

Rais na viongozi hao wawili walijadili maswala yenye umuhimu kati ya Kenya na mataifa yao mbalimbali ikiwemo biashara, uekezaji na uhusiano kati ya raia pamoja na hatua ya Kenya ya kuwania wadhifa usio wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha mwaka 2021 hadi 2022.