Habari

Kenya yaonyesha nia polisi wake kuhudumu Haiti hata muda ukiisha

Na JUSTUS OCHIENG’ May 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KENYA imeonyesha nia ya kikosi chake cha polisi nchini Haiti kuendelea kuhudumu hata baada ya muda wake kumalizika Septemba na imesisitiza tena kujitolea kwake kwa kikosi hicho cha kimataifa kuleta utulivu katika taifa hilo linalohangaishwa na magenge.

Mkuu wa Mawaziri na Waziri wa Masuala ya Kigeni na Wakenya walio nje ya nchi, Musalia Mudavadi, amesema operesheni hiyo inaendelea vizuri, kwa msaada mkubwa wa kimataifa kwa lengo la kurejesha utulivu.

Katika mahojiano maalum na Taifa Leo, Bw Mudavadi alisema Kenya inashirikiana kwa karibu na Umoja wa Mataifa ili kuleta utulivu nchini Haiti, taifa ambalo limeharibiwa na misukosuko ya kisiasa, ghasia za magenge, na kusambaratika kwa utawala wa sheria.

“Operesheni inaendelea,” alisema Bw Mudavadi kuhusu kikosi hicho.

“Tunashirikiana na Umoja wa Mataifa kutoa vifaa kwa polisi nchini Haiti.”

Kwa mujibu wa Bw Mudavadi, Umoja wa Mataifa pesa kwa hazina maalum kusaidia shughuli za kikosi hicho, huku Amerika ikitoa msaada wa kifedha na kidiplomasia.

Amerika pia imetangaza rasmi kuwa magenge nchini Haiti ni sehemu ya mashirika yanayohusishwa na ugaidi, jambo ambalo linatoa fursa ya kuchukuliwa hatua kali za kimataifa.

“Mojawapo ya hakikisho tulilopata kutoka Amerika ni msaada wa kuendelea kwa Kenya kuongoza kikosi hicho Haiti,” alisema Bw Mudavadi.

Muda wa sasa wa kuhudumu kwa kikosi hicho unatarajiwa kuisha Septemba 2025, lakini hatima yake itategemea jinsi jamii ya kimataifa itakavyojibu hali inayoendelea nchini Haiti.

“Hili lilikuwa suala la kimataifa,” alieleza Mudavadi.

“Sasa liko tena mikononi mwa Umoja wa Mataifa, na Katibu Mkuu tayari amewasilisha ombi na ripoti kuhusu hatua zinazofuata,” alisema.