Habari

Kesi ya OCS na sajini walioshtakiwa kwa kudhulumu mahabusu yasambaratika

Na RICHARD MUNGUTI September 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

ALIYEKUWA mkuu Kituo cha Polisi cha Eastleigh Inspekta Rebecca Njeri Muraya aliachiliwa huru katika kesi ya kudhulumu na kutesa mahabusu baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga kusema hakuna ushahidi.

Inspekta Muraya alishtakiwa pamoja na Sajini Abdisalam Ahmed ambaye pia aliondolewa mashtaka.

Akiwaachilia Insp Muraya na Sajini Ahmed, hakimu mkuu mahakama ya Milimani Lucas Onyina, alisema “DPP ameieleza korti kwamba ushahidi alionao hauwezi kuthibitisha kesi dhidi ya maafisa hao wa polisi.”

Wawili hao walikabiliwa na shtaka kwamba mnamo Desemba 31, 2021 katika kituo cha polisi cha Eastleigh North waliamuru Ayni Hussein Mahammud akamatwe na kuzuilwa kwa lengo la kumdhulumu.

Insp Muraya na Sajini Ahmed walidaiwa waliagiza Ayni Hussein Mahammud azuiliwe katika kituo cha polisi cha Muthaiga kwa siku mbili mfululizo.

Bw Onyina alisema DPP ameieleza korti amesoma na kutathmini faili tano za uchunguzi wa kesi hiyo na kufikia uamuzi “hakuna ushahidi wa kutosha kuthibitisha madai walimzuilia Ayni Hussein Mahamud kwa lengo la kumtesa na kumdhulumu.”

Akiwaachilia huru, Bw Onyina alisema mahakama imetilia maanani maungamo ya DPP kwamba hakuna ushahidi wa kutosha kuthibitisha kesi dhidi ya Insp Muraya na Sajini Ahmed.

Pia alisema maafisa hao wawili walikuwa wameadhibiwa na kitengo cha nidhamu- (IAU).

“Kusikiza kesi hii ilhali DPP ameungama hakuna ushahidi wa kutosha ni kuwadhulumu washtakiwa hawa,” Bw Onyina alisema.

Akaendelea kusema,”upande wa mashtaka kupitia kwa Naibu Mkurugenzi Jacinta Nyamosi umefichua hakuna ushahidi wa kutosha na hakuna haja ya kumnyima DPP ombi la kufutilia mbali kesi hii chini ya sheria nambari 87 (a) ya sheria za kupambana na uhalifu (CPC).”

Hakimu alisema ombi la DPP liko na mashiko kisheria na kuwaachilia huru Insp Muraya na Sajini Ahmed.