Kesi ya ujenzi wa kanisa ikulu yavutia kundi
CHAMA cha Wataalamu Wakristo Kenya (KCPF) kimewasilisha ombi kortini kikitaka kujiunga na kesi inayopinga ujenzi wa kanisa ndani ya Ikulu.
Kesi hiyo, iliyowasilishwa na Transparency International Kenya, Kenya Human Rights Commission, Inuka Kenya Ni Sisi na Institute of Social Accountability, inadai mradi huo wa Sh1.2 bilioni unakiuka misingi ya kikatiba ya kutenganisha dini na serikali na pia dhana ya nchi isiyokumbatia dini yoyote.
Katika ombi lake la kutaka kujiunga na kesi hiyo, KCPF—chama kinachowakilisha wataalamu Wakristo kutoka madhehebu mbalimbali kinasema ushiriki wake ni muhimu kwa sababu kesi hiyo inahusu masuala ya msingi wa imani, utamaduni na uongozi.
“Kesi hii inagusa moja kwa moja Ibara ya 32 ya Katiba kuhusu uhuru wa kuabudu, Ibara ya 11 kuhusu kutambua tamaduni, na Ibara ya 45 kuhusu familia. Masuala haya yako ndani ya majukumu ya mwombaji kama mtetezi wa maadili ya kikatiba yanayotokana na imani, familia na utaratibu wa kimaadili,” KCPF inasema katika stakabadhi zake za mahakama.
KCPF inadai kuwa, ikiwa mwakilishi wa Wakenya wengi Wakristo ambao ni asilimia 85.5 ya idadi ya watu, kutoshiriki katika kesi kutanyima mahakama mtazamo muhimu kuhusu uhuru wa dini chini ya Ibara ya 32.