HabariSiasa

Keter na Bowen katika mtanziko baada ya Jubilee kupanga kuwanyima tiketi

March 4th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na JEREMIAH KIPLANG’AT

Kwa ufupi:

  • Alfred Keter na mwenzake wa Kongogo Bowen hawaelewani na Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto
  • Duale asema Jubilee itafanya uchunguzi wa kina kuhakikisha kuwa watakaoteuliwa kuwania hawakatiliwa na IEBC
  • Bw Kangogo amewahi kutangaza wazi kwamba yuko tayari kugura chama cha Jubilee akisema kinamdhibiti kupita kiasi
  • Bw Keter asema anaadhibiwa kwa kukaidi msimamo wake wa kutomheshimu Bw Ruto

HUENDA wabunge wawili waasi wa Jubilee ambao ushindi wao katika uchaguzi uliopita ulibatilishwa na mahakama wakalazimika kutetea viti vyao kwa tiketi ya vyama vingine kwani chama hicho kinapanga kuwanyima udhamini.

Mbunge wa Nandi Hills Alfred Keter na mwenzake wa Marakwet Mashariki Kongogo Bowen hawaelewani na vinara wa chama hicho Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto baada kupokonywa nyadhifa za uongozi katika kamati za bunge la kitaifa mwezi Februari.

Wawili hao sasa watalazimika kusaka kushiriki uchaguzi mdogo kwa udhamini ya vyama visivyo na ushawishi katika maeneo bunge yao.
Baada ya kufutiliwa mbali kwa ushindi wake, Bw Keter alifichua kwamba kuna mpango wa kumnyima tikiti ya Jubilee lakini akabainisha kuwa hatabembeleza mtu yeyote kwa tiketi hiyo.

“Tumeanza safari yetu. Kuna njama ya kuninyima tiketi ya Jubilee. Nafahamu hilo. Hatari ni kwamba nikishiriki mchujo wa Jubilee nitanyimwa ushindi. Nitawapa mwelekeo hivi karibuni,” mbunge huyo mbishani akasema.

Akiongea alipoongoza mkutano wa kundi la wabunge wa Jubilee katika Ikulu ya Nairobi majuzi, Rais Kenyatta alibainisha wazi kuwa chama hicho hakiko tayari kufanya kazi na watu ambao wanataka kuhujumu chama hicho.

 

Onyo

Aliwaonya wabunge wa Jubilee dhidi ya kukwepa mikutano yake huku akiwataka maafisa wa kuwaadhibu wale ambao watadiriki kwenda kinyume na msimamo wa chama hicho.

Japo Kiongozi wa Wengi Aden Duale alisema Jubilee haitamfungia nje yeyote, alisisitiza kuwa watafanya uchunguzi wa kina kuhakikisha kuwa watakaoteuliwa kuwania wadhifa kwa chama hicho hawakatiliwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Akiashiria kuwa itakuwa vigumu kwa Bw Keter kupata tiketi ya chama hicho tawala, Bw Duale alisema makosa ya uchaguzi ni mabaya na atakayepatwa na kosa hilo hawezi kupata idhini yake.

“Hatutazuia mtu yeyote kusaka tiketi ya chama cha Jubilee lakini kabla ya kupewa, kiwango chake cha maadili kitachunguzwa. Makosa ya uchaguzi ni kati ya masuala ya uadilifu ambayo tutazingatia kwa makini,” akaeleza Bw Duale aliye Mbunge wa Garissa Mjini.

Kwenye uamuzi wake mnamo Alhamisi wiki iliyopita, Jaji wa Mahakama Kuu ya Eldoret Kanyi Kimondo alisema alipata ushahidi kuwa Bw Keter aliendesha kampeni nje ya muda uliowekwa na IEBC. Vilevile, jaji huyo aliagiza afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kuchunguza uamuzi wake ili kuamua ikiwa mbunge huyo anafaa kushtakiwa kwa makosa ya uchaguzi.

 

Adhabu

Hata hivyo, japo Bw Keter alisema anaheshimu aumuzi wa mahakama, alisema haridhiki kuwa ulikuwa sahihi. Alisema anaadhibiwa kwa kukaidi msimamo wake wa kutomheshimu Bw Ruto.

Kwa upande wake, Bw Kangogo amewahi kutangaza wazi kwamba yuko tayari kugura chama cha Jubilee akisema kinamdhibiti kupita kiasi.
Lakini baada ya ushindi wake kufutiliwa mbali na Jaji Kimondo alisema yuko tayari kukabiliana na hasidi wake wa kisiasa, Bi Jebii Kilimo katika uchaguzi mdogo.

Hata hivyo, hakutaja chama atakachotumia kushiriki kinyang’anyiro hicho.