Habari

'Kieleweke' na 'Tangatanga' wachafua hewa ya BBI

January 29th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

CHARLES WASONGA na BENSON MATHEKA

WABUNGE wa mirengo ya Tangatanga na Kieleweke sasa wameelekeza vita vya Jubilee katika Mpango wa Maridhiano.

Jumanne, malumbano kati ya wabunge hao yaliendelea pale ‘Kieleweke’ walio mrengo wa Rais Uhuru Kenyatta walipodai kuwa wenzao wa ‘Tangatanga’ waliokutana Naivasha juzi wanahujumu BBI.

Nao wabunge wa ‘Tangatanga’ wanaounga mkono Naibu Rais William Ruto walimkaripia Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju kwa kudai mkutano wa Naivasha haukutambuliwa na chama hicho.

Wakiongea na wanahabari katika majengo ya bunge, Kiongozi wa Wachache John Mbadi, Kiranja wa Wachache Junet Mohamed na Mbunge wa Kieni Kanini Kega walidai ‘Tangatanga’ hawana nia ya kuunga mkono BBI.

Naye Bw Mbadi aliwasuta jumla ya wabunge 100 wa mrengo wa ‘Tangatanga’ akidai waliwahadaa Wakenya kuwa walikuwa wakijadili masuala ya BBI ilhali azma yao kuu ni kuihujumu.

Walipokutana Naivasha, ‘Tangatanga’ walitangaza kuwa wataandaa mikutano ya kuhamasisha umma kuhusu ripoti ya BBI kivyao. .

“Tutaanza mikutano ya kuendeleza uhamasisho kuhusu mapendekezo ya BBI mnamo Februari 8 mjini Nakuru,” akasema kiongozi wa wengi katika Seneti Kipchumba Murkomen.

Hii ni licha ya kuwa mrengo huo ulitangaza wiki iliyopita kuwa utashirikiana na wenzao wa ‘Kieleweke’ katika mikutano ya kuhamasisha, na hata baadhi yao wakahudhuria mkutano ulioandaliwa Mombasa mnamo Jumamosi.

Akimjibu Bw Tuju, Seneta wa Nandi Samson Cherargei alidai Katibu Mkuu wa Jubilee anashirikiana na watu wanaotaka kusambaratisha chama hicho.

“Tuju anatetea maslahi ya ODM na anashirikiana na maadui wanaotaka kuua Jubilee. Wanaogopa kwa sababu Jubilee kimekuwa chama cha kisiasa chenye nguvu na maarufu kote nchini,” akasema Bw Cherargei.

Naye Bw Murkomen alisema mkutano huo haungekuwa wa kundi la wabunge wa Jubilee kwa sababu pia ulihudhuriwa na wabunge wa vyama vingine.