Habari

'Kieleweke' waunga mapendekezo ya BBI

November 29th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

KUNDI la wabunge wa mrengo wa ‘Kieleweke’ limemtaka Rais Uhuru Kenyatta aunde kamati maalum itakayoongoza mchakato wa utekelezaji wa ripoti ya BBI.

Wakiongea na wanahabari Alhamisi katika majengo ya bunge, Nairobi wabunge hao watapatao 25 walisema kamati hiyo itatambua mapendekezo ambayo sharti yatekelezwe kupitia marekebisho ya Katiba ili utaratibu huo uanze “haraka iwezekanavyo”.

“Kamati hiyo pia itabaini mapendekezo ambayo yanahitaji kutekelezwa na asasi mbalimbali za serikali. Kisha, asasi hizo zishurutishwe kuyatekeleza haraka iwezekanavyo,” wabunge hao wakasema kwenye taarifa iliyosomwa, kwa niaba yao na Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa kaunti ya Homa Bay Gladys Wanga.

Huku wakiwataka Wakenya kuisoma ripoti hiyo wao wenyewe ili waelewe yaliyomo na kufanya uamuzi wa busara, wabunge hao walionya wanasiasa wenzao dhidi ya kutumia ripoti hiyo kuendeleza siasa za kutetea masilahi yao.

“Tunatoa wito kwa Wakenya kumiliki ripoti hii ili isinyakuliwe na baadhi ya wanasiasa wenzetu wenye nia mbaya. Hii ni ripoti ya Wanjiku,” taarifa hiyo ikasema.

Miongoni mwa waliotia saini taarifa hiyo ni; Ngunjiri Wambugu (Nyeri Mjini), Gathoni Wa Muchomba (Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Kiambu), Godfrey Osotsi (Mbunge Maalum, ANC), Ruweidha Obbo (Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Lamu), Daniel Maanzo (Makueni, Wiper), Joshua Kuttuny (Cherangany), Gladwell Cheruiyot (Mbunge Mwakilishi Baringo), Simba Arati (Dagoretti Kaskazini, ODM) miongoni mwa wengine.

Wabunge hao hata hivyo walipongeza mapendekezo kwenye ripoti hiyo wakisema yanalenga kuboresha maisha ya Wakenya kwa ujumla.

“Kwa mfano, tunapongeza mapendekezo kama vile msamaha wa ulipaji ushuru, kwa miaka saba, kwa biashara zinazomilikiwa na vijana, kuongezwa kwa mgao wa fedha kwa kaunti hadi kufikia asilimia 35, udumishaji wa kanuni ya mtu mmoja kura moja na watumishi wa serikali kuzuiwa kufanya biashara,” akasema Gladys Wanga kwa niaba yao.