Kifungo cha miaka 35 jela kwa polisi waliotesa na kuua bodaboda aliyekosa kuvalia barakoa
MAHAKAMA Kuu jijini Eldoret imewahukumu maafisa wawili wa polisi kutumikia kifungo cha miaka 35 jela baada ya kupatikana na hatia ya kumtesa hadi kumuua mhudumu wa boda boda, 31 kwa madai ya kukosa kuvaa barakoa mnamo 2020 wakati wa janga la Covid-19.
Jaji Reuben Nyakundi aliwahukumu Emmanuel Wafula, 38, na Godfrey Sirengo, 35, kwa mauaji ya Dennis Lusava.
Wakati akitoa hukumu hiyo, Jaji Nyakundi alisikitika kwamba wawili hao, walikuwa na jukumu la kulinda maisha, lakini badala yake waliamua kuyakatiza.
Mahakama iliambiwa kuwa washtakiwa walimfunga pingu marehemu kwenye dirisha la seli za polisi kabla ya kumtesa hadi akaaga dunia akiwa chini ya ulinzi wao.
Upande wa mashtaka uliambia mahakama kuwa maafisa hao wa zamani waliubeba mwili wa marehemu kwenye gunia na kuutupa katika Mto Nzoia kwenye mpaka wa kaunti za Bungoma na Kakamega.
Katika uamuzi wake, Jaji Nyakundi alibainisha kuwa upande wa mashtaka ulithibitisha pasipo shaka kuwa maafisa hao walimuua Bw Lusava.
Upande wa mashtaka kupitia kwa wakili wa serikali, Sidi Kerengo uliwasilisha mashahidi 21 waliotoa ushahidi dhidi ya washtakiwa hao wakiwemo wazazi wa mhasiriwa, Bw Safani Malongo na Bi Agnes Ambale.
Wazazi wa mwanamume aliyeuawa walipongeza mahakama kwa uamuzi huo, wakiwashukuru mawakili wa Shirika la Kimataifa la Haki za Binadamu (IJM) kwa msaada wao wakati wa kesi hiyo.
“Tunafuraha kwa mahakama kwa kutupa haki baada ya miaka mitano,” alisema Bi Ambale.
“Kama isingekuwa msaada wa mawakili waliojitolea kutuunga mkono, tusingekuwa hapa leo,” aliongeza.
Marehemu aliacha watoto wawili, wasichana wenye umri wa miaka tisa na 14, mtawalia.
Jaji Nyakundi aliwaambia washtakiwa kwamba walichokifanya ni unyama, na kuwaweka watoto hao wawili kwenye uchungu wa kumpoteza baba yao wakiwa na umri mdogo.
Mawakili kutoka IJM walisema mbali na kesi hiyo wanafuatilia kesi zaidi ya 50 ambapo askari polisi wametuhumiwa kuua raia wakiwa chini ya ulinzi wao.