KIHIKA MASHAKANI: Kesi kortini kutaka serikali ya Nakuru ivunjwe, uchaguzi ufanywe
MWANAHARAKATI mmoja wa Nakuru ameanzisha mchakato wa kuvunjwa kwa serikali ya kaunti hiyo kwa sababu ya uwepo wa ombwe la uongozi.
Mhandisi Evans Kimori, ambaye pia ni mkazi wa kaunti hiyo, ameanzisha kampeni ya ukusanyaji sahihi kufanikisha lengo hilo kwa mujibu wa hitaji la Kipengele cha 192 (b) cha Katiba.
Kulingana na kipengele hicho, Rais anaweza kusitisha utendakazi wa serikali ya kaunti endapo kutatokea hitaji la dhararu kama vile kutoelewana miongoni mwa viongozi “au hali nyingine yoyote.”
Kabla ya hatua hiyo kuchukuliwa tume huru itabuniwa kuchunguza madai dhidi ya serikali husika, Rais kuridhishwa na sababu hiyo baada ya seneti kuiidhinisha.
Hatua hiyo ikifaulu, uchaguzi mpya wa magavana na madiwani utafanywa ndani ya siku 90.
Mhandisi Kimori aliwasilisha barua kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) mnamo Aprili akiomba mwelekeo kuhusu msingi wa sheria wa kufanikisha hatua kama hiyo.
Aliomba ithibati kuhusu idadi ya wapiga kura katika kaunti ya Nakuru, idadi ya sahihi inayohitajika na taratibu za kisheria zinazopasa kuzingatiwa katika kuendesha shughuli hiyo.
Kulingana na Mhandisi Kimori, amechukuwa hatua hiyo baada ya bunge la kaunti ya Nakuru kufeli kutekeleza wajibu wake wa kufuatilia utendakazi serikali hii na Gavana Susan Kihika kutokuwa kazini kwa muda mrefu.
Kulingana na mwanaharakati huyo, madiwani wa bunge hilo wametekeleza wajibu wao kuhakikisha kuwa serikali ya Bi Kihika inawajibika kwa wananchi.
Vile vile, Mhandisi Kimori anasema kuwa Gavana Kihika aliondoka na kuelekea Amerika bila kupeana rasmi mamlaka ya kuendesha serikali ya kaunti hali ambayo imesababisha mvutano katika ya Naibu Gavana David Kones na Katibu wa Kaunti Samuel Mwaura.
“Wakazi wa Nakuru wanahitaji uongozi unaowajali, unaoshughulikia matakwa yao na unaowajibika kwao. Inasikitisha kuwa taswira iliyoko katika kaunti ya Nakuru wakati huu ni ile ya kutelekezwa na kufeli kwa ukaguzi wa utendakazi,” akaeleza.
Hii sio mara ya kwanza ambayo Kimori ametaka uongozi wa kaunti ya Nakuru kuonyesha uwajibikaji.
Mnamo Machi 25, mwaka huu aliwasilisha ombi katika Bunge la Kaunti ya Nakuru ikilitaka kuwagiza gavana au mwakilishi wa serikali yake kufika mbele yake kuelezea kutokuwepo kwake kwa muda mrefu na afichue yule ambaye ameshika usukani.
Mhandisi Kimori hajapata majibu rasmi tangu wakati huu.