Kilichomng'oa meno na kucha simba wa Ford-Kenya chabainika
Na WAANDISHI WETU
Kwa ufupi:
- Hali yake ya kujiona kuwa wa hadhi ya juu kutokana na kuwa kinara mwenza katika NASA kulifanya maseneta kumtimua
- Maseneta walalamika Bw Wetang’ula amelemewa kutetea maslahi yao kwenye seneti, wasema huo ni msiba wa kujitakia
- Spika Lusaka apuuzilia mbali barua kutoka kwa NASA ikieleza kuwa muungano umemdumisha Bw Wetang’ula kama kiongozi wa wachache
- Bw Musyoka na Mudavadi waendelea kumtetea simba wa Ford- Kenya wakihofia hatua ya kumtimua itapasua NASA
SENETA wa Bungoma Moses Masika Wetang’ula Jumanne alivuliwa wadhifa wa Kiongozi wa Wachache katika Seneti kutokana na kile baadhi ya maseneta wa Muungano wa NASA walisema ni kushindwa kutetea maslahi yao.
Taifa Leo pia ilifahamishwa kuwa hali yake ya kujiona kuwa wa hadhi ya juu kutokana na kuwa kinara mwenza katika NASA sawa na Raila Odinga, Kalonzo Musyoka na Musalia Mudavadi pia ilifanya maseneta kuamua kumteremsha madaraka.
Ingawa wengi waliona hatua hiyo kama iliyochochewa na hatua ya ODM kuamua kushirikiana na Serikali ya Jubilee, Kiranja wa Wachache katika Seneti, Bw Mutula Kilonzo (Makueni) alieleza kuwa mambo hayo mawili ndiyo yaliyommaliza Bw Wetangula.
Mwiba wa kujichoma
“Ndugu Wetang’ula ameanguka kutokana na sababu za kujitakia. Msiba wa kujitakia hauna pole. Maseneta wenzake wamekuwa wakilalama tangu mwaka jana kuwa hawawezi kumfikia,” akasema Bw Mutula ofisini mwake kabla ya kikao cha kumbadua.
Maseneta hao walihisi kuwa Bw Wetang’ula hakuwa akiwasilisha maslahi yao kwa Spika Ken Lusaka ambaye pia anatoka kaunti ya Bungoma, kwa kuwa anaamini ni mwanasiasa wa tajriba ya juu ikilinganishwa na Bw Lusaka, na hivyo hangeweza kunyenyekea limbukeni.
“Hapa hakuna suala la chama cha ODM. Ni maslahi ya maseneta wa upinzani wanaomuona Bw Wetang’ula kuwa anayejali ukubwa wake katika NASA kuliko mahitaji ya wenzake katika Seneti.
Jumanne, maseneta 19 wa NASA walimchagua mwenzao wa Siaya, James Orengo kuchukua nafasi ya Bw Wetang’ula. Seneta wa Kakamega, Cleopa Malala alichaguliwa naibu wa Bw Orengo.
“Kipindi cha kuhudumu cha Seneta Moses Wetang’ula kama Kiongozi wa Wachache Seneti kimeisha mara moja na Seneta James Aggrey Orengo anatambuliwa kuanzia sasa kama Kiongozi wa Wachache,” Spika Lusaka alieleza Seneti.
Barua ya NASA haitabadilisha chochote
Bw Lusaka alipuuzilia mbali barua kutoka kwa afisa mkuu wa NASA, Norman Magaya ambayo ilieleza kuwa muungano umemdumisha Bw Wetang’ula kama kiongozi wa wachache.
Spika Lusaka alisema mawasiliano yalistahili kutoka kwa Kiranja wa Wachache, ambaye ni Seneta Mutula wala sio kutoka nje.
Jumanne, chama cha Ford-Kenya, anachokiongoza Bw Wetang’ula kilitaja hatua hiyo kama isiyokiyumbisha kwani utaratibu ufaao wa kisheria haukuzingatiwa.
Kwenye kikao wa wanahabari jijini Nairobi, viongozi wa chama hicho walisema kwamba hawatambui hatua hiyo, kwani kulingana na mwafaka wa muungano wa NASA, chama kimoja hakiwezi kudai kumwondoa mwanachama mmoja kutoka cheo fulani.
Kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi alieleza kusikitishwa na kile alichosema ni njama za ODM kumhangaisha Bw Wetang’ula.
Naye Bw Musyoka alisema uamuzi wa kumteua Bw Wetangula nafasi ya kiongozi wa wachache bungeni, ilikuwa ya vinara wakuu wa NASA na wala si ODM.
Ripoti za WYCLIFFE MUIA, WANDERI KAMAU, CHARLES WASONGA na LUCY KILALO