Habari

Kilio cha wakulima wa miwa

October 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na IAN BYRON na CHARLES WASONGA

WAKULIMA wa miwa wametisha kufanya maandamano makubwa katika makao makuu ya Wizara ya Kilimo jijini Nairobi kuishinikiza serikali kushughulikia matatizo yao.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Wakulima wa Miwa Nchini Ezra Olodi alisema wakulima watatumia maandamano hayo ambayo yameratibiwa kufanyika wiki ijayo kuwasilisha malalamishi ya kile wanachodai ni kushindwa kwa serikali kuokoa kampuni za sukari ambazo zinaendela kusambaratika.

Alisema maafisa wa shirikisho hilo tayari wamewasilisha ombi rasmi kwa Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai la kutaka waruhusiwe kufanya, kuongoza na kushiriki maandamano ya amani.

“Tutafanya maandamano katika makao makuu ya Wizara ya Kilimo kuitaka iingilie kati madhila yetu kama wakulima wa miwa nchini, ambayo yamechangiwa na kuporomoka kwa kampuni za kubwa za sukari katika maeneo kunakokuzwa sukari kwa wingi nchini,” akasema Bw Olodi.

Katibu huyo Mkuu alilikashifu jopokazi lililoteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta kushughulikia masuala yanayoathiri wakulima wa miwa kwa kutowasilisha ripoti yake, mwaka mmoja baada ya kuundwa. Jopokazi hilo linaongozwa na Wazii wa Kilimo Mwangi Kiunjuri na Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya.

“Maandamano yetu yanalenga kuikumbusha Wizara ya Kilimo kwamba wakulima hawajaridhishwa na jinsi inavyoshughulikia matatizo yetu. Tunataka kuona ripoti ya jopokazi lililoteuliwa kushughulikia malalamishi ya wakulima na changamoto zinazoikumba sekta ya sukari nchini kwa ujumla,” akasema Bw Olodi.

Akaongeza: “Inasikitisha kuwa kampuni za sukari ambazo zinamilikiwa na serikali zinaelekea kusambaratika ilhali serikali inaendelea kutoa mazingira bora kwa wafanyabiasha kuagiza sukari kutoka nje. Hali hii inawavunja moyo wakulima ambao sasa wanahangaika wasijue pa kupeleka miwa yao.”

Ilani hiyo ya kufanya maandamano inajiri wiki mmoja baada ya nyingine kama hiyo iliyotolewa na muungano wa wakulimwa wa miwa katika eneo ya SoNy kufutiliwa mbali kutoa nafasi kwa mashauriano miongoni mwa wadau.

Wakati huu kampuni kubwa za sukari humu nchini zinazongwa na changamoto za ukosefu wa fedha za kulipia madeni, mishahara ya wafanyakazi na kugharamia uendeshaji wa shughuli za kawaida pamoja na kukarabati mitambo yao.

Kampuni ya Sukari ya Mumias sasa imewekwa chini ya mrasimu aliyeteuliwa na Benki ya Kenya Commercial baada ya kushindwa kulipa deni la Sh24 bilioni inayodaiwa na benki hiyo.

Hali ni mbaya kiasi kwamba baadhi ya viongozi kutoka eneo hilo wanaiomba serikali kuingilia kati kukifufua kiwanda hicho.

Ijumaa, Seneta wa Kaunti ya Kakamega, Cleophas Malala ameitaka KCB kuhakikisha kwamba haiuzi kiwanda hicho kwa kile ametaja ni “kisingizio cha kuwa chini ya mrasimu.”

Naye Mwakilishi wa Wanawake wa kaaunti ya Kakamega katika Bunge la Kitaifa, Elsie Muhanda ameitaka serikali ifanye kulihali kunasua kampuni hiyo.

Na akaunti za kampuni ya SoNy iliyoko Awendo wiki jana zilifungwa na Kamishna wa Vyama vya Ushirika kwa kufeli kuwasilisha fedha inazokata kutoka kwa mishahara ya wafanyakazi wake kama michango yao ya kila mwezi kwa vyama vya ushirika.