Kimataifa

Mahakama yakubali kesi kuhusu Trump kukataa uraia wa watoto

Na BENSON MATHEKA, MASHIRIKA December 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Mahakama ya Juu ya Amerika imekubali kusikiliza kesi kuhusu iwapo baadhi ya watoto wanaozaliwa Amerika wana haki ya kikatiba ya kupewa uraia.

Siku yake ya kwanza ofisini mwezi Januari, Rais Donald Trump alisaini agizo la kusitisha utoaji wa uraia kwa watu wanaozaliwa nchini humo na wazazi wasio na vibali halali vya kuishi Amerika, lakini hatua hiyo ikazuiwa na mahakama za chini.

Hadi sasa, tarehe ya kusikilizwa kwa kesi hiyo bado haijapangwa, na uamuzi unaweza kutolewa baada ya miezi kadhaa. Uamuzi huo utakuwa na athari kubwa kwa msimamo mkali wa utawala wa Trump kuhusu uhamiaji na dhana nzima ya uraia wa Amerika.

Kwa karibu miaka 160, Marekebisho ya 14 ya Katiba ya Amerika yameweka bayana kuwa mtu yeyote anayezaliwa nchini humo ni raia wa Amerika, isipokuwa watoto wa wanadiplomasia na wanajeshi wa mataifa ya kigeni. Marekebisho hayo yanasema: “Watu wote waliozaliwa au waliohalalishwa Amerika, na walioko chini ya mamlaka yake, ni raia wa Amerika.”

Agizo la Trump linataka kuzuia uraia kwa watoto wa wahamiaji wasio na vibali au walio nchini kwa visa za muda. Ni sehemu ya ajenda pana ya mageuzi ya uhamiaji yanayolenga kukabiliana na kile ambacho utawala huo umeita “tishio kubwa kwa usalama wa kitaifa na usalama wa umma”.

Utawala wa Trump unadai kuwa kifungu cha “walioko chini ya mamlaka yake” kinamaanisha kuwa watoto wa watu wasio na hadhi ya kisheria ya kudumu hawastahili uraia wa kuzaliwa.

Hata hivyo, Cecillia Wang, Mkurugenzi wa Masuala ya Kisheria katika Umoja wa Uhuru wa Kiraia Amerika (ACLU), kinachowakilisha walalamishi, alisema kupitia CBS – mshirika wa BBC – kwamba hakuna rais anayeweza kubadili ahadi ya msingi ya Marekebisho ya 14.

“Kwa zaidi ya miaka 150, imekuwa sheria na utamaduni wetu wa kitaifa kwamba kila anayezaliwa katika ardhi ya Amerika ni raia,” alisema.

Amerika ni miongoni mwa takriban nchi 30 – hasa za Amerika – zinazotoa uraia kwa yeyote anayezaliwa ndani ya mipaka yake.

Baada ya changamoto nyingi mahakamani, majaji kadhaa wa shirikisho walikataa agizo hilo, wakisema linakiuka Katiba, na mahakama mbili za rufaa zikaendeleza amri ya kulizuia kutekelezwa. Trump alikata rufaa hadi Mahakama ya Juu, ambayo mwezi Juni ilisema mahakama za chini zilikwenda mbali kupita mipaka yao katika kutoa agizo hilo—ingawa haikutoa uamuzi kuhusu hoja ya uraia wa kuzaliwa.

Marekebisho ya 14 yalipitishwa baada ya Vita vya wenyewe kwa wenyewe ili kutoa ufafanuzi wa uraia wa watumwa walioachiliwa, waliokuwa wamezaliwa Amerika.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, D John Sauer, amesema marekebisho hayo yalinuia kuwapa uraia watumwa waliokuwa wamekombolewa pamoja na watoto wao—si watoto wa wageni waliokuwa Amerika kwa muda au wasio na vibali. Alisema kuna “mtazamo usio sahihi” kwamba kuzaliwa katika ardhi ya Amerika kunatosha kupewa uraia, na akaonya kuwa dhana hiyo imeleta “athari mbaya”.