Rais wa Guinea Bissau akamatwa siku tatu baada ya uchaguzi, wanajeshi watangaza mapinduzi
Rais wa Guinea-Bissau Umaro Sissoco Embaló Jumatano alikamatwa na watu wenye silaha, vyanzo vya serikali vilisema kufuatia milio ya risasi karibu na Ikulu ya Rais.
Baadaye kundi la maafisa wa jeshi lilitangaza kwamba lilitwaa uongozi wa serikali ya Guinea-Bissau, taifa ambalo limekumbwa na mapinduzi mara kadhaa, baada ya milio ya risasi kusikika katika maeneo muhimu ya mji mkuu, Radio France Internationale iliripoti.
Maafisa hao wa jeshi walisema wameunda “Uongozi wa Juu wa Kijeshikwa Kurejesha Utulivu” na kwamba wataongoza nchi hiyo ya Afrika Magharibi hadi taarifa nyingine itakapotolewa.
Hatua hiyo imejiri siku moja kabla ya tume ya uchaguzi kutangaza matokeo ya awali ya uchaguzi wa urais uliokuwa na ushindani mkali kati ya Rais Umaro Sissoco Embaló na mpinzani mkuu Fernando Dias. Pande zote mbili zilidai ushindi katika duru ya kwanza ya uchaguzi uliofanyika Jumapili.
Walioshuhudia walisema milio ya risasi ilisikika karibu na makao makuu ya tume ya uchaguzi, Ikulu ya Rais na Wizara ya Mambo ya Ndani. Risasi zilidumu kwa takriban saa moja kabla ya kukoma karibu saa kumi na moja saa za eneo la magharibi mwa Afrika, mwandishi wa Reuters alishuhudia.
Mapema Jumatano, wanajeshi walichukua udhibiti wa barabara kuu inayoelekea Ikulu, na kutawanya watu na magari yaliyokuwa yakikimbia eneo hilo wakiogopa machafuko.
Jeshi lilitangaza kuwa limechukua “udhibiti kamili” wa nchi, likasitisha mchakato wa uchaguzi na kufunga mipaka ya taifa hilo, ikiwa ni siku tatu tu baada ya uchaguzi wa wabunge na urais katika nchi hiyo masikini ya Afrika Magharibi.
Taarifa hiyo ilisomwa katika makao makuu ya jeshi jijini Bissau na kushuhudiwa na wanahabari wa AFP.
Matokeo rasmi ya muda yalitarajiwa kutolewa Alhamisi katika nchi ambayo tangu kupata uhuru wake imekumbwa na mapinduzi manne ya kijeshi na majaribio mengine kadhaa ya kuipindua serikali.
Hadi kufikia Jumatano asubuhi, uchaguzi ulikuwa umefanyika kwa amani, huku Embaló akitarajiwa kushinda. Hata hivyo, chama kikuu cha upinzani PAIGC na mgombea wake Domingos Simões Pereira hawakuruhusiwa kushiriki katika uchaguzi huo baada ya Mahakama ya Juu kusema waliwasilisha stakabadhi zao kwa kuchelewa.
Pereira na Embaló ni mahasimu wa muda mrefu; uchaguzi wa urais wa 2019 ulisababisha mzozo wa miezi minne baada ya wote kudai ushindi.
Kiongozi wa ujumbe wa waangalizi wa ECOWAS, Issifu Baba Braimah Kamara, Jumanne alikuwa amesifu uchaguzi akisema ulifanyika kwa “amani na utulivu”—kabla ya machafuko ya Jumatano.
Guinea-Bissau ni miongoni mwa nchi masikini zaidi duniani na imekuwa kitovu cha biashara ya dawa za kulevya kati ya Amerika ya Kusini na Ulaya, biashara inayochochewa na historia yake ndefu ya hali ya kuyumba kwa kisiasa.
Mmoja wa wapita njia waliokuwa wakikimbia eneo la tukio alisema kwa majonzi: “Tumezoea hali kama hii hapa Bissau.”