Trump asema Amerika imemkamata Rais Maduro wa Venezuela
Rais wa Amerika Donald Trump amesema kuwa Ameria ilifanya “shambulio kubwa” dhidi ya Venezuela na kumkamata Rais wa nchi hiyo, Nicolas Maduro, pamoja na mke wake.
Hii ni taarifa kamili aliyochapisha kupitia mtandao wa Truth Social:
“Amerika imefanikiwa kutekeleza shambulio la kiwango kikubwa dhidi ya Venezuela na kiongozi wake, Rais Nicolas Maduro,pamoja na mke wake, wamekamatwa na kusafirishwa nje ya nchi.
Operesheni hii ilifanywa kwa ushirikiano na vikosi vya Usalama za Amerika. Maelezo zaidi yatatolewa baadaye. Kutakuwa na mkutano na wanahabari leo saa 11 asubuhi katika Mar-a-Lago. Asanteni kwa kuzingatia suala hili! Rais DONALD J. TRUMP.”
Serikali ya Venezuela ilisema mashambulizi pia yalifanyika katika majimbo ya Miranda, Aragua na La Guaira, hali iliyomlazimu Rais Maduro kutangaza hali ya dharura kitaifa na kuandaa vikosi vya ulinzi.
Milipuko, ndege za kivita na moshi mzito mweusi vilionekana katika maeneo mbalimbali ya Caracas kuanzia takriban saa nane usiku kwa muda wa dakika 90, kulingana na waliozungumza na Reuters na picha zilizosambaa mitandaoni.
Katika jiji zima, raia wa Venezuela walionekana kushtuka na kuingiwa na hofu waliponasa video za moshi mkubwa na miale ya rangi ya chungwa angani. “Mpenzi wangu, hapana, tazama hiyo,” alisema mwanamke mmoja katika video, akishangaa milipuko iliyoonekana kwa mbali.
Walioshuhudia walisema kukatika kwa umeme kuliathiri eneo la kusini mwa jiji, karibu na kambi kubwa ya kijeshi.
Trump ameahidi mara kwa mara kuendesha oparesheni za ardhini katika nchi hiyo ya Amerika Kusini inayozalisha mafuta, ambayo imekuwa ikiongozwa na Maduro tangu 2013.
Amerika, upinzani nchini Venezuela na mataifa mengine kadhaa wanasema Maduro alidanganya katika uchaguzi uliofanyika mwaka jana ili kubaki madarakani.
Ingawa Trump hajataja wazi malengo yake, Reuters imeripoti kuwa kwa siri amekuwa akimshinikiza Maduro aondoke nchini humo. Mnamo Jumatatu, Trump alisema itakuwa “busara” kwa Maduro kuacha madaraka.
Pentagon ilielekeza maswali ya Reuters Ikulu ya White House, ambayo ilikataa kutoa maoni.
Katika taarifa yake, serikali ya Venezuela ilisema lengo la mashambulizi hayo ni Amerika kujipatia mafuta na madini ya nchi hiyo, lakini ikaongeza kuwa “haitafanikiwa” kuchukua rasilmali hizo.
Amerika imeongeza kwa kiasi kikubwa wanajeshi wake katika eneo hilo, ikiwemo meli ya kubeba ndege za kivita, manowari na ndege za kisasa za kivita zilizo katika Bahari ya Caribean.
Trump amekuwa akishinikiza Venezuelew kuwekewa “vizuizi” vya mafuta , kuongeza vikwazo dhidi ya serikali ya Maduro, na amefanya zaidi ya mashambulizi 24 dhidi ya vyombo vya majini ambavyo Amerika inadai vilihusika katika biashara ya dawa za kulevya katika Bahari ya Pacific na Carebean.
Wiki iliyopita, Trump alisema Amerika ilishambulia eneo nchini Venezuela ambako mashua hupakia dawa za kulevya, hatua iliyotajwa kuwa mara ya kwanza Washington kufanya shambulizi la ardhini nchini humo tangu kampeni dhidi ya Maduro ilipoanza.