Kimemramba Mackenzie, sasa yuko kwenye tanuri ya moto
MAHAKAMA Kuu jana ilimpata mhubiri matata Paul Mackenzie na washukiwa wenzake 30 na hatia ya kushirikiana, kutekeleza na kudumisha mfungo uliosababisha vifo vya mamia ya watoto na watu wazima katika msitu wa Shakahola, Kilifi.
Katika uchambuzi wake wa mashtaka 191 ya mauaji, Jaji Diana Kavedza alisema vifo hivyo vilisababishwa na vitendo na uzembe usio halali wa watu waliotekeleza na kudumisha mfungo huo, badala ya kuwa matokeo yasiyokusudiwa ya shughuli za kidini.
“Baada ya kuzingatia ushahidi wote, mahakama hii imebaini kuwa washtakiwa ambao ushiriki wao binafsi umethibitishwa walitenda kwa pamoja utekelezaji wa lengo moja lisilo halali la kuanzisha na kudumisha mfungo uliosababisha vifo vya watu wengi Shakahola,” akasema Jaji Kavedza.
Jaji huyo alibaini kuwa ingawa kila mshtakiwa alikuwa na jukumu tofauti, vitendo vyao vilikuwa sehemu ya mpango mmoja wa uhalifu. Hata hivyo, kila mmoja alipaswa kuwajibishwa kwa msingi wa ushahidi unaoonyesha ushiriki wake na nia yake ya kutenda uhalifu.
Kabla ya kuchambua mashtaka ya mauaji, mahakama pia ilibainisha kuwa ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka uliibua maswali kuhusu uwezekano wa vitendo hivyo kuchukuliwa kama uhalifu dhidi ya binadamu.
Jaji Kavedza alikataa hoja kwamba watoto waliofuata maagizo na kuendelea kufunga hadi kufa walikuwa wameamua kufanya hivyo kwa hiari yao wenyewe.
Alisema watoto wenye umri wa kati ya miaka sita na 10 hawakuwa na uwezo wa kutafakari kwa kina na kuelewa kuwa kifo ni cha kudumu. Mawazo yao, tabia ya kutenda bila kufikiria na uelewa wao mdogo viliwafanya kuwa rahisi kudanganywa.
“Kwa hivyo, inawezekana watoto katika kundi hili, kutokana na msisimko wa shahidi huyu, licha ya kuonekana kama mifupa iliyofunikwa kwa ngozi, waliamini kuwa kifo kinaweza kubatilishwa,” akasema .
Alibaini kuwa watoto hao hawangeweza kutoa ruhusa ya hiari, yenye ufahamu na inayokubalika kisheria ya kujinyima chakula hadi kufa.
Mahakama ilisema kutokupinga maagizo au kukubali mafundisho hayo hakumaanishi kuwa watoto walikuwa wameamua kufa kwa hiari. Badala yake, mwenendo wao ulipaswa kuangaliwa katika mazingira ya imani za kidini, utegemezi kwa watu wazima, mamlaka ya wazazi, udanganyifu, hofu na shinikizo.
“Mahakama imebaini kuwa vifo vilivyosababishwa na njaa vilitokana na vitendo au uzembe usio halali wa wale waliotekeleza mfumo wa mfungo,” akasema Jaji Kavedza.
Mashahidi wa upande wa mashtaka walisema kuwa katika mikutano ya maombi chini ya miti Shakahola, Mackenzie aliwaambia wafuasi kuwa Yesu hangekuja kuwaelekeza kufunga hadi kufa ili waende mbinguni.
Ushahidi ulionyesha kuwa wazazi waliagizwa kuwanyima watoto wao chakula, kabla ya kuanzishwa kwa mfungo mkavu uliokataza wafuasi kunywa maji. Maagizo hayo yalihusu waumini wote, wakiwemo watoto ambao hawakuwa na uwezo wa kuelewa kikamilifu matokeo yake.
Jaji alisema maagizo hayo yalikuwa ya lazima, huku juhudi zikifanywa kuzuia wafuasi kuacha mfungo. Hali hiyo ilikuwa muhimu katika kutathmini nia ya washtakiwa. Alisema maelezo ya kidini yaliyotolewa kuhalalisha mfungo hayangeondoa moja kwa moja nia ya kutenda uhalifu. Mahakama ilipaswa kuchunguza nia ya vitendo hivyo, kwani lengo la kiroho halimaanishi kuwa mtu hawezi kuwa na nia ya kusababisha kifo.
Vifo vilivyoendelea kutokea na hali ya wafuasi kudhoofika kimwili pia vilizingatiwa. Mfungo uliendelea licha ya dalili za wazi za madhara yake.
Mahakama pia ilichunguza ushahidi kwamba nguvu zilitumiwa kuwalazimisha wafuasi kutii na kuwazuia watu wa nje kuwafikia waliokuwa wakifunga.
Njia za kuingia katika baadhi ya makazi zilifungwa kwa matawi na miiba, huku wahanga waliodhoofika kwa njaa wakiachwa bila msaada.
Mnamo Machi 23, 2023, shahidi wa upande wa mashtaka aliingia msituni akiwa na waandishi wa habari. Alisema Julius Katana alimtishia, huku mshtakiwa mwingine akimshika shingoni na kumkandamiza chini.Wengine walidaiwa kumpiga na kumsababishia majeraha kichwani na kwenye mbavu.
Washukiwa hao wanatarajiwa kurejea mahakamani Novemba 6 kwa ajili ya kusikilizwa kwa hoja kuhusu hukumu watakazopewa.
Shahidi mwingine alithibitisha tukio hilo, ambalo liliripotiwa katika Kituo cha Polisi cha Lango Baya. Upande wa mashtaka pia uliwasilisha ushahidi kuhusu kushambuliwa kwa afisa wa Shirika la Huduma kwa Wanyamapori Kenya (KWS) aliyeingia msituni.
Jaji alisema matukio hayo yalikuwa muhimu katika kutathmini iwapo mfungo ulidumishwa kwa vitisho, vizuizi na vurugu, na kama washukiwa walielewa matokeo ya vitendo vyao.
Ushahidi kutoka kwa Msajili wa Mashirika ulionyesha kuwa Mackenzie alikuwa mkuu wa Good News International Ministries, huku mshtakiwa wa pili akiwa katibu.
Mashahidi walisema Mackenzie aliongoza mikutano chini ya miti Shakahola na kutoa maagizo kwa waumini. Baada ya kanisa na kituo cha televisheni cha Times Television kufungwa, aliwaambia wafuasi kuwa kanisa lilikuwa likihamia Shakahola, akitaja eneo hilo kama “Kanisa Jangwani”.
Mackenzie alihusishwa na maagizo ya kuwalazimisha wafuasi kufunga, huku baadhi ya mashahidi wakieleza kuhusu kupigwa na matumizi ya mijeledi dhidi ya waliopinga.
Baada ya kutathmini ushahidi wote, jaji alisema washukiwa ambao ushiriki wao binafsi ulithibitishwa walitenda kwa pamoja kutekeleza na kudumisha mfungo uliosababisha vifo hivyo.
“Nimeridhika kuwa upande wa mashtaka umethibitisha kesi yake bila kuacha shaka ya msingi. Kwa hivyo, kila mshtakiwa anapatikana na hatia katika mashtaka yote 191 ya mauaji na anatiwa hatiani kama alivyokuwa ameshtakiwa,” akasema Jaji.
Washukiwa hao wanatarajiwa kurejea mahakamani baadaye kwa ajili ya kusikilizwa kwa hoja kuhusu hukumu watakazopatiwa.