Habari

Kinachofanya shule kupokonywa uhifadhi wa vyeti vya KCSE

Na SAMWEL OWINO October 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KUANZIA mwaka ujao, wanafunzi wanaohitimu Kidato cha Nne hawatakuwa wakichukua vyeti vyao vya mtihani wa Kenya Certificate of Secondary Education (KCSE) kutoka shule zao, bali katika ofisi za elimu za kaunti ndogo.

Waziri wa Elimu, Bw Julius Ogamba, aliambia Bunge kuwa hatua hiyo inalenga kukomesha tabia ya wakuu wa shule kuwazuia wanafunzi kupata vyeti vyao kwa sababu ya madeni ya karo, licha ya serikali kupiga marufuku jambo hilo mara kadhaa.

“Badala ya mivutano ya kila mara kati ya wanafunzi na wakuu wa shule, kwa nini Baraza la Mitihani la Kenya (KNEC) lisitume vyeti moja kwa moja kwa wanafunzi, kama vile vyeti vya kuzaliwa vinavyopatikana kupitia E-Citizen?” alihoji Mbunge wa Funyula, Dkt Wilberforce Oundo.

Bw Ogamba alikubaliana na hoja hiyo, akisema kuwa matokeo yajayo ya KCSE yatasambazwa kwa ofisi za elimu za  kaunti ndogo, huku nakala za orodha za wanafunzi zikipelekwa shuleni kwa uthibitisho.

“Hii itasaidia kuhakikisha hakuna changamoto ambapo wanafunzi wanaendelea kuteseka au kulazimishwa kulipa gharama za ziada ili wapate vyeti vyao,” alisema Bw Ogamba.

Kwa mujibu wa Sheria ya Baraza la Mitihani la Kenya ya 2012, kipengele cha 10(1b), hakuna mtu wala taasisi inayoruhusiwa kushikilia cheti cha mwanafunzi kwa sababu yoyote ile.

“Vyeti au diploma zilizotolewa na baraza hazipaswi kuzuiliwa kwa sababu yoyote,” sheria hiyo inasema.

Hata hivyo, licha ya maagizo haya ya serikali, wakuu wa shule wameendelea kushikilia vyeti vya wanafunzi hadi walipe salio la karo, hali ambayo imekuwa ikiathiri maisha ya wahitimu wengi.

Mwenyekiti wa Muungano wa Wakuu wa Shule za Sekondari (KESSHA), Bw Willy Kuria, alikaribisha uamuzi huo, akisema wakuu wa shule hawana pingamizi.

“Tatizo kubwa ni kuwa wanafunzi wenyewe huwa hawaji kuchukua vyeti. Changamoto inaweza kuwa kwa ofisi za elimu kuhifadhi vyeti hivyo salama kwa muda mrefu,” alisema Bw Kuria.

Alisema baadhi ya vyeti vimehifadhiwa shuleni tangu miaka ya 1960 na 70, hata kabla ya baadhi ya wakuu wa sasa kuzaliwa.

Kulingana na Bw Kuria, wanafunzi wengi hutumia taarifa za matokeo kujiunga na vyuo vikuu na vya kati, na hurudi kuchukua vyeti halisi baadaye.

“Watakapoanza kwenda kwa maafisa wa elimu kwa wingi, kutakuwa na msongamano na usumbufu mkubwa,” aliongeza.