Habari

Kindiki asihi Raila, Ruto wazidi kushirikiana hata baada ya pigo AUC

Na CECIL ODONGO February 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

NAIBU wa Rais Prof Kithure Kindiki ametoa wito kwa viongozi waendelee kuungana chini ya Rais William Ruto na Kinara wa Upinzani Raila Odinga hata kama taifa lilikosa kuwahi uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).

Bw Odinga alibwagwa na mwenyekiti mpya wa AUC, Mahmoud Ali Youssef, raia wa Djibouti, kwenye kura iliyoandaliwa jijini Addis Ababa, Ethiopia, Jumamosi.

Hii ni licha ya kuongoza kampeni kali na kuzunguka Afrika nzima, Rais Ruto akiwa mstari wa mbele kumvumisha kwa viongozi wa mataifa.

“Tunaomba rais wetu, waziri mkuu wa zamani na viongozi wote waendelee kushirikiana kujenga Kenya mpya, na kuhakikisha kuna amani na umoja nchini,” akasema Prof Kindiki.

“Tunastahili kuendelea kufanya kazi pamoja jinsi ambavyo tumekuwa tukifanya wakati wa kampeni za AUC,” akaongeza.

Alikuwa akiongea katika kanisa la Methodist la Nkubu, Imenti Kusini, Kaunti ya Meru, katika hafla ya kumtawaza Kasisi Stephen Mawira, kwenye sherehe iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kisiasa kutoka kaunti hiyo.

Katika ibada hiyo, Prof Kindiki alisema kuwa atakutana na gavana, wabunge, madiwani na zaidi ya wawikilishi 3,000 kutoka kaunti hiyo hapo Jumanne katika makazi yake mtaani Karen, Nairobi.

Alifafanua kuwa mkutano huo hautakuwa wa kisiasa ila wa kujadili jinsi ambavyo serikali kuu inavyoisadia kaunti hiyo kupata miradi ya maendeleo.

“Hautakuwa mkutano wa kisiasa bali tutakuwa tukijadili miradi ya maendeleo ya Kaunti ya Meru hasa maji, kawi, barabara miongoni mwa kazi nyingine,” akaongeza Prof Kindiki aliyelifu kanisa la Methodist kwa kazi nzuri linayofanya.