Habari

Kindiki: Mimi sio mtu wa kufunzwa kazi na wapinzani wangu, na mimi si mwoga

Na DAVID MUCHUI February 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

NAIBU Rais Kithure Kindiki amewaonya wapinzani wake wa kisiasa dhidi ya kudharau uwezo wake akisisitiza kuwa yeye sio mwoga.

Naibu Rais alisema wapinzani wa kisiasa walikuwa wakijaribu kila mara “kumfundisha kazi yake” na akawapuuza akisema kwamba anafahamu wazi majukumu yake.

Prof Kindiki alizungumza wakati wa mkutano na viongozi wa Kaunti ya Meru katika makazi yake Karen, Nairobi uliofanyika Jumanne.

Alisema hawezi kufuata nyayo za mtangulizi wake Rigathi Gachagua ambaye alidai alijikita katika kumpinga rais badala ya kuwa msaidizi mkuu wa kiongozi wa nchi.

“Baadhi ya watu wanajaribu kunifundisha jinsi ya kufanya kazi yangu lakini siwezi kuwa upinzani serikalini. Ninaelewa wajibu wangu na nitafaulu mtihani wangu kwa kishindo,” Profesa Kindiki alisema.

Bw Kindiki alisema analenga kumsaidia Rais William Ruto kutekeleza ajenda yake ya maendeleo kote nchini.

Aliwaambia wakosoaji ambao alisema wanamtaka kuzingatia eneo analotoka badala ya nchi yote.

“Kuna watu wanadhani tunaogopa kuzungumzia tunakotoka. Hatuhitaji kutenga maeneo mengine ya Kenya ili kuendeleza nyumbani.

Marehemu rais wa zamani Mwai Kibaki alifanya mengi katika eneo lake bila kutangaza alikotoka,” alisema.

Aliongeza: “Sitazunguka nchi nzima kutangaza jinsi ninavyopenda eneo la Mlima Kenya. Vitendo kama hivyo vitavuruga hali ya amani nchini.”

Prof Kindiki alisema Serikali Jumuishi sasa itaanza kuzindua miradi ambayo itafadhiliwa kikamilifu.

Naibu rais alisema Rais Ruto hatishwi na wale wanaodai atahudumu kwa muhula mmoja.

“Kuna siasa nyingi za kuwasisimua raia. Kazi ya mabadiliko haifurahishi lakini wengi wanapenda sarakasi za aina hiyo,” alisema.