Kindiki roho juu kwamba UDA itashinda uchaguzi mdogo Mbeere Kaskazini
NAIBU Rais Profesa Kithure Kindiki ameeleza matumaini yake kuwa UDA itashinda kiti cha ubunge cha Mbeere Kaskazini kwenye uchaguzi mdogo utakaondaliwa baada ya mchakato wa kubuni Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC) kukamilishwa.
Profesa Kindiki alisema hisani pekee ambayo wapigakura wa eneobunge hilo wanaweza kufanya ni kumchagua mbunge wa UDA baada ya Geoffrey Ruku kuteuliwa waziri wa Utumishi wa Umma.
“Nitapiga kambi hapa Mbeere Kaskazini kumpigia debe mwaniaji wa UDA kwa sababu kiti hiki ni cha chama tawala,” akasema Profesa Kindiki.
Alikuwa akiongea katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Siakago Kaunti ya Embu wakati ambapo alikutana na zaidi ya wazee 5,000, mkutano ambao uliratibiwa na Bw Ruku.
“Nasubiri siku ambayo IEBC itatangaza siku ya uchaguzi ili nije Mbeere kufanya kampeni. Kwa sababu wadhifa wa uwaziri ulirejea Mbeere hisani ni kupatia chama tawala pia ubunge,” akaongeza.
Tayari wawaniaji wanane wameonyesha nia ya kuwania ubunge wa Mbeere Kaskazini kwa tikiti ya UDA. Profesa Kindiki alisema wanane hao watapitia mchujo ambapo mshindi ndiye atapeperusha bendera ya chama hicho.
“Watu wataamua nani atakuwa mwaniaji wa UDA nasi hatutavuruga uteuzi. Tuna watu wanane ambao wanamezea mate kiti hiki na wale ambao watashindwa, wanastahili kumuunga mkono mshindi atwae kiti hiki,” akasema.
Bw Ruku alisema wazee kutoka koo mbalimbali eneo hilo wamekubali kusimama na mwaniaji wa UDA wakati wa uchaguzi huo mdogo.
“Wazee hao wameungana na wanaongea kwa sauti moja,” akasema Bw Ruku.
Waziri huyo alisema serikali imeanzisha miradi mbalimbali Mbeere na wakazi hawatabanduka serikalini.
“Tumeona kile ambacho serikali imetufanyia na tutasalia tuonyeshe uaminifu wetu kabisa,” akasema Bw Ruku.
Profesa Kindiki alisisitiza kuwa serikali ina pesa za kutosha na miradi yote ambayo imekwama itafufuliwa na kukamilishwa kabla ya 2027.
“Uchumi unaendelea kuimarika na kama serikali tutahakikisha tunatimiza ahadi zetu,” akaongeza.
Awali akiwahutubia wakazi wa Kerugoya, Kaunti ya Kirinyaga, Profesa Kindiki aliambia upinzani imakinikie miradi ya maendeleo badala ya kueneza siasa za mgawanyiko.
“Tunawaambia wapinzani wetu kwamba ni mapema sana kufanya kampeni kwa kura ya 2027,” akasema Profesa Kindiki.