Kinoti, Wetang’ula watofautiana kuhusu dhahabu feki
Na LEONARD ONYANGO
MKURUGENZI wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) George Kinoti ametofautiana na Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula kuhusu mwaliko wa kumtaka kuandikisha taarifa kuhusiana na dhahabu feki.
Bw Kinoti, alishikilia kuwa Bw Wetang’ula alifaa kuandikisha taarifa kuhusiana na sakata inayomkabili kuhusu biashara ya dhahabu feki
“Ni ukweli, Bw Wetang’ula alifaa kuandikisha taarifa leo,” akasema Bw Kinoti aliyekuwa ameandamana na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji walipokuwa wakihutubia wanahabari katika hoteli ya Serena, Nairobi.
Bw Wetang’ula, hata hivyo anashikilia kwamba hajapokea mwaliko wowote kutoka kwa DCI.
Kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetang’ula alipokuwa akihutubia wanahabari mapema Jumatano alipuuzilia taarifa zilizodai kwamba amealikwa kwenda kuandikisha taarifa kwa DCI kuhusiana na sakata ya dhahabu feki.
“Sakata hiyo hainishtui mimi,” akasema Bw Wetang’ula.
“Mimi nilikuwa na mkutano na viongozi wa chama cha Ford Kenya na nikitoka hapa naenda kufariji familia ya aliyekuwa mbunge wa Amagoro Fredrick Oduya Oprong,” akasema Seneta wa Bungoma.
Oprong aliaga dunia Jumamosi akiwa na umri wa miaka 83.
Awali, kulikuwa na madai kwamba Bw Wetangula alitarajiwa mapema Jumatano kufika katika makao makuu ya DCI kuandikisha taarifa kuhusiana na sakata ya dhahabu bandia.
Wiki iliyopita, Idara ya DCI ilisema kuwa tayari imeharifiwa kuhusiana na sakata hiyo na tayari imeanzisha uchunguzi ili kuwanasa waliotekeleza ulaghai huo.
Bw Wetang’ula amejipata pabaya baada ya kanda ya sauti kuchipuza katika mitandao ya kijamii ambapo amesikika akizungumza na mfanyabiashara kutoka Dubai kuhusu shehena ya dhahabu inayodaiwa kuzuiliwa na serikali katika Uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA).
Katika kanda hiyo Bw Wetang’ula anasikika akiahidi kuzungumza na kiongozi wa ODM Raila Odinga, Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i ili shehena hiyo iachiliwe.
Bw Haji alisema anangojea faili kutoka kwa DCI kabla ya kuchukua hatua.