Kitendawili cha mwanafunzi kutekwa nyara akielekea kufanya mtihani wa KCSE
MWANAFUNZI wa Kidato cha Nne katika Shule ya Upili ya Mseto ya St Philips, Kaunti ya Kirinyaga, alinusurika kifo baada ya kutekwa nyara na watu wasiojulikana alipokuwa akielekea kufanya mtihani wa kitaifa wa KCSE mnamo Novemba 3, 2025.
Wycliffe Muthii, mwenye umri wa miaka 17, alikuwa amejitayarisha kufanya karatasi ya Kiingereza na Kemia, lakini safari yake ya kuelekea kituo cha mtihani ilikatizwa na majambazi waliomvamia, wakamdunga dawa ya kumlewesha na kumtupa ndani ya gari kabla ya kuondoka naye.
Baada ya kutekwa, Muthii alikosa kufanya karatasi mbili za mtihani, jambo lililomuacha akiwa ameshtuka na mwenye hofu.
Kulingana na wazazi wake, Bw Julius Wamugunda na Bi Mercy Wambura, mwana wao alirauka alfajiri, akala kifungua kinywa na kuanza safari kuelekea shule, bila kujua kilichokuwa kinamsubiri.
“Inasikitisha sana. Tulipokea simu kutoka kwa kituo cha mtihani tukielezwa kuwa mwana wetu hakuwa amewasili. Hatuwezi kuelezea uchungu tulioupata,” alisema Bw Wamugunda.
Muda mfupi baadaye, walimu wa shule walifika nyumbani kwao kijijini Kiaga kuuliza alikokuwa mwanafunzi huyo. Wazazi walieleza kuwa alikuwa ameondoka saa kumi na mbili asubuhi akielekea shuleni.
Habari za kutoweka kwa mwanafunzi huyo zilienea haraka, na wanakijiji walianza msako mkali. “Tulimtafuta kila mahali kijijini lakini hatukumuona,” alisema mama yake, Bi Wambura.
Baada ya saa kadhaa, familia ilipokea taarifa kuwa kijana huyo alikuwa ameokolewa na alikuwa katika kituo cha polisi cha Makuyu, Kaunti ya Murang’a, baada ya kutupwa porini na watekaji wake.
“Alipozinduka, alijikuta porini na kupiga mayowe akiomba msaada. Bahati nzuri, alisaidiwa na msamaria mwema aliyempeleka kituo cha polisi cha Makuyu,” alisema shangazi yake, Bi Roselyn Warui.
Baadaye alikimbizwa katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Sagana ambako alipokea matibabu na kuruhusiwa kuondoka.
Wazazi wake walisema wanaamini watekaji walinuia kumharibia mwana wao maisha kwa kumfanya akose kufanya mitihani. “Wamefanikiwa kwa sehemu, maana alikosa mitihani miwili muhimu,” alisema Bw Wamugunda kwa huzuni.
Hata hivyo, walifurahia kuona akirudi akiwa salama na aliweza kurejea shuleni Jumanne kuendelea karatasi za mitihani zilizosalia.
Wazazi hao wametaka polisi kuchunguza kisa hicho kwa kina na kuwakamata wahalifu waliohusika. “Tunataka uchunguzi wa kina na wahusika wachukuliwe hatua kali za kisheria,” alisema Bw Wamugunda.