Habari

Kitengo maalum chabuniwa kukabili madereva watukutu barabarani

Na GITONGA MARETE December 17th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KITENGO maalum kimeundwa na kutumwa kukabiliana na madereva wanaokiuka sheria wakati wa msimu wa sikukuu.

Hatua hiyo inalenga kudhibiti ongezeko la ajali za barabarani, Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja alisema jana.

Akitoa tangazo hilo Jumatatu, Desemba 15, 2025, Mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Haki za Utawala (NCAJ), Jaji Mkuu Martha Koome alisema mahakama za kuhamishwa pia zitaanzishwa kwenye barabara kuu kote nchini, ambapo wakosaji watatozwa faini papo hapo.

Kitengo hicho kinajumuisha maafisa wa polisi, Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama (NTSA), Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) pamoja na Idara ya Mahakama.

Bw Kanja aliwaonya madereva kuwa yeyote atakayepatikana akikiuka sheria za trafiki atachukuliwa hatua kali, akisema idadi inayoongezeka ya ajali wakati wa msimu wa sikukuu inatia hofu.

Alisema kitengo hicho kitakabiliana na uendeshaji hatari wa magari na vitendo vya ufisadi ili kuhakikisha Wakenya wako salama.