Konstebo apotea katika tukio lisiloeleweka Lamu
Na KALUME KAZUNGU
IDARA ya usalama, Kaunti ya Lamu imeanzisha operesheni ya kumsaka afisa wa polisi aliyetoweka katika hali tatanishi siku mbili zilizopita.
Hesbon Okemwa Anunda ambaye ni afisa wa polisi wa cheo cha konstebo alikuwa akihudumu kwenye kituo kidogo cha polisi cha Tchundwa, Kaunti Ndogo ya Lamu Mashariki na aliripotiwa kupotea tangu Jumatano alfajiri akiwa njiani kutoka Kizingitini kuelekea Tchundwa.
Ripoti za polisi ziliarifu kuwa Bw Anunda alikuwa na bunduki aina ya G3 pamoja na risasi 60 na alionekana na mmoja wa maafisa wa polisi waliokuwa wakishika doria kwenye kituo cha Tchundwa saa kumi na moja na nusu alfajiri.
“Alitoka hapa kituoni saa kumi na moja na nusu alfajiri na alikuwa amebeba bunduki yake aina ya G3 na risasi zipatazo 60. Baadaye tuliarifiwa kuwa afisa huyo kati ya Kizingitini na Tchundwa. Hatujui aliko kwa sasa,” akasema mmoja wa maafisa wa polisi ambaye alidinda kutaja jina lake.
Katika kikao na wanahabari ofisini mwake Ijumaa, Kamanda wa Polisi, Kaunti ya Lamu, Bw Muchangi Kioi alithibitisha kutoweka kwa afisa huyo na kusema kuwa msako kumpata afisa huyo pamoja na bunduki na risasi alizobeba unaendelea.
Aomba ushirikiano
Bw Kioi aliwataka wakazi kushirikiana na walinda usalama katika kumsaka afisa huyo ambaye hali yake haijulikani kwa sasa tangu kutoweka kwake.
“Ni kweli. Mnamo Jumatanio, Oktoba 2, 2019, saa kumi na moja na nusu hivi, mmoja wa maafisa wangu aliyehudumu kwenye kituo kidogo cha polisi cha Tchundwa alitoweka akiwa njiani kutoka Kizingitini kuelekea Tchundwa. Ningeweaomba wananchi wenye taarifa kumhusu kutusaidia ili kujua aliko. Tayari msako mkali dhidi ya afisa huyo unaendelea kote Lamu Mashariki na viungani mwake hadi pale polisi huyo, bunduki na risasi alizokuwa nazio zipatikane,” akasema Bw Kioi.
Si mara ya kwanza kwa afisa wa polisi kujipata katika sokomoko, kaunti ndogo ya Lamu Mashariki.
Februari 2018, afisa wa polisi wa cheo cha Konstebo, Bw Paul Rotich, aliyekuwa akihudumui kwenye kituo cha polisi cha Kizingitini aliponea chupuchupu pale alipovamiwa na kukatwa kwa mapanga na mtu asiyejulikana.
Bw Rotich alikuwa akinunua chakula na bidhaa nyingine kabla ya uvamizi dhidi yake kutekelezwa na mvamizi aliyeaminika kuwa mhalifu sugu aliyekuwa ameachiliwa baada ya kukamilisha kifungo chake cha miaka mitatu kwenye gereza la Shimo la Tewa mjini Mombasa.
Mnamo Oktoba, 2017, maafisa wa polisi eneo la Faza walilazimika kumpiga risasi na kumuua papo hapo mshukiwa sugu, Hassan Mohamed,27, aliyejaribu kuwashambulia maafisa hao kwa upanga wakati walipokuwa kwenye harakati za kumkamata.