Koome ashauri raia na polisi kuhusu maandamano
JAJI Mkuu Martha Koome ametoa wito wa heshima na tahadhari kati ya wananchi wanaotekeleza haki zao na maafisa wa usalama wanapotekeleza majukumu yao, ili kudumisha demokrasia na uthabiti wa kijamii nchini Kenya.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuwaapisha makamishna wa Tume ya Taifa ya Huduma ya Polisi (NPSC) na mwanachama wa Baraza la Mashujaa wa Kitaifa katika Mahakama ya Juu, Jaji Mkuu Koome alieleza kuwa taifa liko katika kipindi nyeti cha safari yake ya kidemokrasia, ambapo limekumbwa na maandamano ya mara kwa mara ambayo yamejaribu maadili ya kikatiba.
“Maandamano haya yanakumbusha kwamba demokrasia si tu kuwa na haki zilizoandikwa, bali ni jinsi haki hizo zinavyoheshimiwa na kutekelezwa kwa vitendo,” alisema.
Alisisitiza haja ya kudumisha mizani ya heshima, ambapo wananchi wana haki iliyolindwa ya kukusanyika na kuandamana kwa amani, lakini lazima wafanye hivyo bila kutumia vurugu, uharibifu wa mali au vitisho.
“Katika nyakati za hivi karibuni, taifa letu na mshikamano wetu wa kidemokrasia vimekuwa katika hali ya misukosuko kupitia mawimbi ya maandamano ya umma. Vipindi hivi vimetufundisha kuhusu uzito wa kudumisha mizani ya haki kati ya haki ya kikatiba ya maandamano ya amani na umuhimu wa huduma ya polisi inayozingatia utu wa mwananchi,” Jaji Mkuu Koome alieleza.
Wakati huohuo, polisi, wanapaswa kuwa na nidhamu, kuepuka matumizi ya nguvu kupita kiasi, na kuwaheshimu raia wote kwa kuheshimu haki za binadamu na utawala wa sheria.
Ujumbe wa Jaji Mkuu ni wito kwa pande zote mbili: kwa waandamanaji, kubaki kuwa na amani na kutii sheria; na kwa polisi, kuwa na kiasi, haki, na weledi katika utendaji kazi wao.