Habari

Korti yaagiza Mbunge wa Juja George Koimburi akamatwe

Na RICHARD MUNGUTI July 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MBUNGE wa Juja, George Koimburi, atakamatwa kwa kushindwa kufika mahakamani kujibu mashtaka ya kula njama ya kuvuruga haki na kutoa taarifa za uongo kuhusu madai ya kutekwa nyara.

Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Mahakama ya Milimani, Bennark Ekhubi, alitoa amri hiyo baada ya Koimburi na washukiwa wenzake wawili kukosa kufika mahakamani Jumatano, Julai 16. 2025.

Watatu hao wametakiwa kufikishwa mahakamani Agosti 5, 2025 kujibu mashtaka yanayowakabili.

Wakati huo huo, washukiwa wanne waliokuwa wakichunguzwa kuhusiana na madai ya kupanga njama ya Koimburi kujiteka nyara walikana mashtaka matatu dhidi yao.

Washukiwa hao Grace Nduta Wairimu (MCA wa wadi ya Kanyenya-ini), Peter Kiratu Mbari, David Macharia Gatana, na Cyrus Muhia wameshtakiwa kwamba mnamo Mei 25 katika eneo la Mugutha, eneobunge la Juja, walikula njama ya kuvuruga haki kwa kupanga utekaji feki wa Koimburi.

Kulingana na upande wa mashtaka, kitendo hicho kililenga kumzuia Koimburi kukamatwa na kufikishwa katika Mahakama ya Kiambu kujibu mashtaka manne kuhusiana na kesi ya ulaghai wa ardhi, kama ilivyoelekezwa na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kupitia barua ya Mei 20.

Koimburi na Peter Kiratu pia wameshtakiwa kwa kosa la kutoa taarifa za uongo na kuchapisha habari za uongo.

Koimburi, ambaye bado hajajibu mashtaka, anadaiwa kuwa mnamo Juni 7 katika Hospitali ya Karen kupitia akaunti ya YouTube, alitoa taarifa kwa vyombo vya habari akidai kuwa alitekwa nyara na kuteswa na watu wasiojulikana – madai ambayo alijua si ya kweli na yaliyokusudiwa kuzua taharuki kwa umma.

Kiratu kwa upande wake anashtakiwa kuwa mnamo Mei 25 katika Kituo cha Polisi cha Mugutha, alitoa ripoti kwa afisa Nelly Kabuu kwamba Koimburi alitekwa nyara na watu waliovaa barakoa baada ya kuhudhuria ibada katika Kanisa la Full Gospel eneo hilo.

Taarifa hiyo ilisababisha afisa Kabuu kuandika ripoti hiyo kwenye kitabu cha matukio Mei 25, 2025, taarifa ambayo Kiratu alijua si ya kweli.

Mwendesha mashtaka wa serikali, Victor Owiti, hakupinga kuachiliwa kwa washukiwa kwa dhamana, akieleza kuwa tayari walikuwa wameachiliwa kwa dhamana ya pesa taslimu Sh300,000 hapo awali na walishirikiana na wachunguzi.

Mawakili wa utetezi waliambia mahakama kuwa washukiwa wako tayari kutii masharti yoyote yatakayotolewa.

Mahakama iliambiwa kuwa washukiwa hao wamekuwa wakishirikiana vyema na polisi na wameonyesha tabia njema.

Katika uamuzi wake, Hakimu Ekhubi aliwaagiza washukiwa waendelee na dhamana ile ile ya Sh300,000 waliyopewa mwezi Mei 2025, lakini sasa wanahitajika pia kutoa majina ya watu watatu wa kuwawajibikia.

Mahakama pia imeagiza polisi kukamilisha uchunguzi kuhusiana na magari yaliyokamatwa, ambapo ilielezwa kuwa baadhi yake yalikuwa na hundi na hati miliki za ardhi.

Kesi hiyo itatajwa Agosti 5, 2025.