Habari

Korti yafuta kikosi cha washauri wa Ruto

Na JOSEPH WANGUI January 22nd, 2026 Kusoma ni dakika: 2

MAHAKAMA Kuu imebatilisha kuanzishwa kwa ofisi za washauri wa Rais William Ruto, hatua ambayo ni pigo kwa muundo wa serikali jumuishi uliowajumuisha wanasiasa na wataalamu waliokuwa wakihusishwa na vyama vya upinzani.

Katika uamuzi wenye athari pana uliotolewa Alhamisi, Januari 22, 2026, mahakama ilibatilisha kuundwa kwa Ofisi za Washauri wa Rais na kufuta uteuzi wa watu 21 waliokuwa wakihudumu katika nyadhifa hizo.

Mahakama pia ilizuia Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) na Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC) kutambua ofisi hizo au kulipa mishahara na marupurupu yoyote yanayohusiana nazo.

Uamuzi huo ulitokana na kesi mbili zilizowasilishwa na shirika la Katiba Institute pamoja na mwanaharakati wa haki za binadamu wakili Suyianka Lempaa, waliopinga kile walichokitaja kama kurejea kwa “baraza la siri” ndani ya serikali kuu, linalofanya kazi nje ya Katiba na mifumo rasmi ya utumishi wa umma.

Jaji Mwamuye alibaini kuwa ingawa Rais huenda alichukua hatua hizo kwa nia njema, mchakato uliotumika kuunda ofisi za ushauri ulikuwa ni “ukiukaji mkubwa” wa Katiba na sheria.

“Hatua, maamuzi na mapungufu katika mchakato huo yanaonyesha kukiukwa kwa katiba kwa kiwango cha hatari na kisichorekebishika,” aliamua jaji huyo.

Ofisi zilizobatilishwa ni pamoja na Baraza la Washauri wa Masuala ya Uchumi wa Rais, Ofisi ya Mshauri wa Usalama wa Chakula na Uzalishaji wa Mifugo, Huduma za Utekelezaji wa Serikali, Ofisi ya Mshauri wa Usalama wa Taifa, Ofisi ya Mshauri wa Haki za Wanawake na Ofisi ya Baraza la Ushauri wa Mabadiliko ya Tabianchi.

Nyingine ni Ofisi ya Masuala ya Fedha na Sera ya Bajeti, Ofisi ya Mabadiliko ya Kiuchumi, Mshauri wa Masuala ya Mifugo na Malisho, Mshauri Mkuu wa Masuala ya Kikatiba, Mshauri Mkuu wa Kisiasa, Mshauri Maalum wa Uwezeshaji wa Kiuchumi kwa Vijana na Ofisi ya Mshauri Mkuu wa Uchumi.

Miongoni mwa waliokuwa wakinufaika na ofisi hizo tata ni Bw David Ndii, Profesa Makau Mutua, Bw Jaoko Oburu ambaye ni mpwa wa marehemu kiongozi wa ODM Raila Odinga, aliyekuwa Wakili Mkuu Kennedy Ogeto na wakili Harriet Chiggai, miongoni mwa wengine.

Walalamishi walidai kuwa ajira hizo zilisababisha serikali kuwa kubwa kupita kiasi, hali ambayo Wakenya walirekebisha mwaka 2010 kupitia Katiba mpya kwa kuweka idadi ya mawaziri na makatibu wakuu, “ambao wanapaswa kuwa wataalamu na ndio washauri wa Rais.”

Mahakama iliamua kuwa Rais Ruto alipuuza jukumu la lazima la kutoa mapendekezo kwa Tume ya Utumishi wa Umma chini ya Ibara ya 132(4)(a) ya Katiba na hakuzingatia masharti ya kisheria yaliyoainishwa katika Sheria ya Tume ya Utumishi wa Umma na kanuni zake.

Pia ililaumu mchakato huo kwa kutekelezwa bila ushauri wa Tume ya Mishahara na Marupurupu kuhusu athari za kifedha.

Aidha, mahakama ilibaini kuwa ofisi hizo ziliundwa kwa siri bila ushiriki wa umma, kinyume na Ibara ya 10 na 201 za Katiba.

Jaji alisema hilo lilikiuka misingi ya utumishi wa umma ikiwemo uwazi, uadilifu, ushindani wa haki na matumizi bora ya fedha za umma.

“Muundo sambamba wa ushauri usiodhibitiwa na pengine usio wa lazima, ulioundwa kupitia mchakato wa siri, usio na ushindani na usio halali, unakiuka hitaji la Katiba la uwazi, uwajibikaji na utumishi wa umma unaofanya kazi kwa ufanisi,” alisema jaji.

Kutokana na hayo, mahakama ilitangaza ofisi hizo na uteuzi uliotokana nazo kuwa batili tangu mwanzo. Ilitoa maagizo ya kubatilisha maamuzi yote ya kuunda ofisi hizo na kuwateua washauri hao, na kuizuia kabisa serikali kuwezesha au kuwalipa fedha zozote.

Jaji pia alitoa agizo akiitaka PSC, ndani ya siku 90, kufanya ukaguzi wa kina wa ofisi zote zilizoanzishwa katika Ofisi ya Rais tangu kutangazwa kwa Katiba ya 2010, hususan zile zilizoanzishwa chini ya Rais Ruto baada ya Agosti 2022.

Ofisi yoyote itakayobainika kuanzishwa kinyume cha Katiba itavunjwa, huku ripoti ya maendeleo ikitakiwa kuwasilishwa mahakamani ndani ya siku 120.