Korti yakataa kumzuia Lagat kurejea afisini
MAHAKAMA imekataa kumzuia Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Eliud Lagat kurejea afisini.
Jaji Chacha Mwita amesema kwamba kesi iliyowasilishwa inayopinga ufaafu wake kuendelea na wadhifa wake kwa kuhusishwa na mauaji ya mwalimu na bloga Albert Ojwang itaendelea kusikizwa huku Naibu Mkuu huyo wa polisi akiendelea na majukumu yake.
Jaji Mwita ameagiza kwamba wahusika wote kwenye kesi hiyo waandikishe majibu yao hadi Julai 25 ambapo atatoa mwelekeo zaidi kuhusu kesi hiyo.
Bw Lagat alijiondoa afisini mwezi jana kufuatia shinikizo nyingi kutoka kwa umma baada ya Bw Ojwang kupoteza maisha yake akiwa mikononi mwa polisi.
Wengi walihoji kwamba kwa kuwa alikuwa mlalamishi mkuu aliyepelekea Ojwang kukamatwa kwa tuhuma za kumchafulia jina, basi alikuwa anahusika kwa njia moja au nyingine na kifo cha mwalimu huyo akiwa seli za kituo cha polisi cha Central.
Tayari maafisa kadhaa wa polisi wameshtakiwa kwa mauaji ya Ojwang, akiwemo OCS wa Central Samson Talaam.