Korti yamtaka Waititu aendelee kuzoea kunguni wa jela hadi rufaa iamuliwe
ALIYEKUWA Gavana wa Kiambu, Ferdinand Waititu, atakaa gerezani kwa muda mrefu zaidi baada ya kupoteza ombi lake la kuachiliwa kwa dhamana akisubiri rufaa anayopinga kifungo cha miaka 12 jela kwa ufisadi.
Jaji Lucy Njuguna alisema Waititu pamoja na Charles Chege na Mwangi Wahinya hawakutoa masuala ya kisheria ili kuachiliwa kwa dhamana kusubiri rufaa kusikilizwa na kuamuliwa.
Aliafikiana na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kwamba hakuna masuala ya kisheria yaliyoibuliwa na wafungwa hao watatu ili kuwezesha mahakama kuingilia kati.
Alisema sababu za kimatibabu hazitoshi kuwapa dhamana wakisubiri rufaa kwani kuna vituo vya matibabu kushughulikia changamoto zao za kiafya.
“Mahakama haijaridhishwa na sababu za walalamishi kuweza kuwapa dhamana kwa wakati huu,” Jaji Njuguna alisema.
“Kwa hivyo, ombi la dhamana limetupiliwa mbali,” aliamua.
Walalamishi hao watatu walikuwa wamewasilisha maombi ya kuachiliwa kwa dhamana wakisubiri rufaa ya kupinga vifungo vyao jela.
Waititu alipatikana na hatia na kuhukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 12 baada ya kushindwa kulipa faini ya Sh53.5 milioni.
Chege alitozwa faini ya Sh295 milioni au atumikie kifungo cha miaka 11 jela huku Wahinya akitozwa faini ya Sh1 milioni au atumikie kifungo cha miaka saba jela.
Walipatikana na hatia mnamo Februari 14 na hakimu wa Mahakama ya Kupambana na Ufisadi, Thomas Nzioki.
Katika rufaa aliyowasilisha katika Mahakama Kuu ya Kupambana na Ufisadi ya Milimani, Waititu kupitia kwa wakili Danstan Omari alimkashifu hakimu kwa kutochanganua kikamilifu ushahidi aliowasilisha.
Timu yake ya wanasheria inatoa sababu kadhaa za kukata rufaa, ambazo ni pamoja na madai kwamba upande wa mashtaka ulishindwa kufikia kiwango kinachohitajika kuthibitisha kesi, mahakama ilipuuza utata katika kesi, na mashahidi wakuu hawakuitwa kutoa ushahidi.
“Upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha kesi yao kwa kiwango kinachohitajika bila shaka,” karatasi za rufaa zilisema.
Katika rufaa hiyo, Waititu anadai kuwa mahakama hiyo haikuzingatia vya kutosha ushahidi wake au kutoa uchambuzi unaofaa wa utetezi wake.