Korti yaokoa Prof Anangwe dhidi ya shoka la Waziri Ogamba chuoni UoN
MAHAKAMA kuu imefutilia mbali uamuzi wa Waziri wa Elimu Julius Migos Ogamba kumtimua mwenyekiti wa baraza la Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN) Prof Amukowa Anangwe.
Jaji Bahati Mwamuye aliamuru Prof Anangwe aendelee kutekeleza majukumu yake kama mwenyekiti wa baraza hilo la UoN.
Na wakati huo huo Jaji Mwamuye alipiga breki kuteuliwa kwa mtu mwingine yeyote kuteuliwa kutwaa wadhifa huo wa uenyekiti wa baraza la UoN.
Jaji huyo alipiga marufuku tangazo la gazeti rasmi la serikali lililotiwa sahihi na Bw Ogamba likimtimua kazini Prof Anangwe.
“Baada ya kutathmini ushahidi uliowasilishwa na wakili Abdirazak Mohamed, nimeridhika Waziri wa Elimu Julius Migos Ogamba alikaidi sheria alipomwachisha kazi Prof Anangwe bila makosa yoyote,”alisema Jaji Mwamuye.
Jaji huyo alisema Waziri Ogamba alitumia mamlaka yake vibaya kwa kumtimua mamlakani Bw Againe bila idhini.
Jaji huyo alielezwa Bw Ogamba alichapisha katika gazeti rasmi la serikali uamuzi uliokinzana na sheria.
Bw Mohamed alieleza mahakama kwamba sheria imempa Waziri nafasi ya kuteua na haimruhusu kumtimua mwanachama yeyote kutoka kwa baraza hilo.
Jaji Mwamuye alielezwa Prof Anangwe aling’olewa kabla ya muda wake wa kuhudumu miaka mitatu kukamilika.
“Prof Anangwe alikuwa amebakikisha miezi 14 kukamilisha muda wake wa miaka mitatu,” wakili huyo aliambia mahakama kuu.
Jaji Mwamuye aliambiwa Prof Anangwe ni mmoja wa wanafunzi wa zamani wa UoN na kumtimua bila sababu ni kumshushia hadhi yake.
Prof Anangwe alisema amesimishwa wakati ule ameweka mikakati kufufua UoN inayokabiliwa na changamoto za fedha na karibuni itafilisika.
Prof Anangwe alieleza mahakama kwamba chuo hicho kina deni la zaidi ya Sh20 bilioni.
Jaji Mwamuye aliamuru washtakiwa (Ogamba na Mwanasheria Mkuu) wawasilishe majibu mnamo Machi 28, 2025 na kuorodhesha kesi hiyo itajwe Aprili 2, 2025 kwa maagizo zaidi.