Korti yazima jaribio la kushtaki Matiang’i
Na RICHARD MUNGUTI
JARIBIO la mwanahabari Dennis Itumbi kutaka kumfungulia mashtaka ya ufisadi Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i liligonga mwamba Ijumaa, mahakama iliposema hakufuata utaratibu na mwongozo uliowekwa kisheria.
Akitupilia mbali ombi hilo la Bw Itumbi, hakimu mkuu wa mahakama ya kuamua kesi za ufisadi, Bw Douglas Ogoti, alisema mlalamishi hakuambatanisha orodha ya mashahidi na taarifa zao kama inavyotakiwa katika kipengee nambari 89 cha sheria za Uhalifu.
Pia alisema mlalamishi hakufikia malengo yaliyoelekezwa katika katiba.
“Sheria zinazoipa mahakama uwezo wa kumruhusu mwananchi kuwasilisha kesi ya kibinafsi dhidi ya mshukiwa, zimeweka masharti ambayo mtu anastahili kuyatimiza kabla ya kukubaliwa kuwasilisha mashtaka dhidi ya mhusika,” alisema Bw Ogoti.
Alisema amesoma nakala za ushahidi 82 alizoambatisha na ombi lake la kutaka akubaliwe kumshtaki Dkt Matiang’i kwa kashfa ya ununuzi wa shamba lenye thamani ya Sh1.5 bilioni kutoka kwa Bw Francis Mburu katika eneo la Ruaraka, Nairobi.
Dkt Matiang’i anadaiwa kukaidi sheria alipokuwa waziri wa Elimu kwa kutumia pesa za umma vibaya kununua ardhi kinyume na mwongozo wa sheria uliowekwa.
Hakimu huyo alisema Bw Itumbi aliandikia asasi kadhaa za serikali nyaraka akiomba ushahidi aliotarajia kuutegemea katika kesi hiyo dhidi ya waziri huyo wa zamani wa Elimu.
Mahakama ilisema “hakuna chembe ya ushahidi kuthibitisha kuwa Bw Itumbi alifanya jitihada zozote kusaka ushahidi kutoka kwa idara mbalimbali za serikali, zilizohusika na ununuzi wa shamba hilo lililo na thamani ya mabilioni ya pesa”.
Punde tu baada ya ombi hilo kuzamishwa kisheria, Bw Itumbi alimweleza Bw Ogoti kuwa atawasilisha rufaa kupinga hatua hiyo ya kumnyima fursa ya kutenda haki.