Habari

Korti yazima mazishi ya mtawa aliyeuawa kanisa likishtakiwa

Na DAVID MUCHUI November 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MAHAKAMA Kuu mjini Meru imesitisha mazishi ya Mtawa wa Kanisa Katoliki, marehemu Anselmina Karimi, aliyeuawa mwezi uliopita, hadi kesi iliyowasilishwa na mmoja wa warithi wake isikilizwe na kuamuliwa.

Jaji Stephen Githinji alitoa amri hiyo Jumatano na kuelekeza kuwa stakabadhi za kesi ziwasilishwe kwa washtakiwa wote kwa muda wa siku nne.

“Kabla ya kusikilizwa na kuamuliwa kwa kesi hii, amri ya muda inatolewa dhidi ya washtakiwa wa kwanza na wa pili, maajenti wao, wawakilishi au mtu yeyote anayefanya kazi kwa niaba yao, kuendelea, kuidhinisha au kuwezesha mazishi ya marehemu Mtawa Anselmina Karimi yaliyopangwa kufanyika Alhamisi, Novemba 6, 2025 au tarehe nyingine yoyote.”

Mlalamishi katika kesi, Bw Thomas Murithi Mwiraria, anayenufaika na Makao ya Watoto ya Meru taasisi iliyokuwa ikisimamiwa na Mtawa Karimi, adai Kanisa lilipanga kumzika marehemu bila kumshirikisha yeye, familia yake, au watoto waliokuwa chini ya malezi ya marehemu.

Bw Mwiraria, ambaye alilelewa katika kituo hicho cha watoto yatima, ameshtaki Kanisa Katoliki Jimbo la Meru, Shirika la Watawa wa Nazareth Sisters of Annunciation, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Hospitali ya Consolata Nkubu na Waziri wa Usalama wa Ndani na Utawala wa Kitaifa.

Anadai kuna wasiwasi mkubwa kuwa mazishi yangefanyika kabla ya uchunguzi wa kina wa kisayansi kukamilika.Mahakama imepanga kutaja kesi hiyo Novemba 13 2025.