Korti yazima uajiri wa makurutu wa polisi uliopaswa kuanza Ijumaa
USAJILI wa makurutu wa polisi 10,000 kote nchini uliopangwa kuanzia Ijumaa, Oktoba 3, 2025 umesitishwa na Mahakama ya Leba kufuatia mvutano kuhusu nani kati ya Inspekta Jenerali wa Polisi na Tume ya Huduma ya Polisi (NPSC) ana mamlaka ya kuendesha zoezi hilo.
Mwanasiasa John Harun Mwau aliwasilisha kesi akidai kuwa Katiba ya Kenya inatambua Huduma ya Polisi (NPS) kuwa chini ya uongozi huru wa Inspekta Jenerali wa Polisi, na kwamba hakuna mtu au chombo chochote chenye mamlaka ya kumuagiza kuhusu masuala ya ajira, uhamisho, upandishaji vyeo, kusimamishwa kazi au kufutwa kazi kwa maafisa wa polisi.
Jaji Hellen Wasilwa wa Mahakama ya Mahusiano ya Ajira na Kazi alitoa amri ya muda ya kuzima usajili huo, uliokuwa uanze Oktoba 3, hadi pale kesi hiyo itakaposikilizwa na kuamuliwa kikamilifu.
“Amri ya muda inatolewa kusitisha zoezi zima la usajili hadi kesi hii itakapoamuliwa,” alisema Jaji Wasilwa.
Katika ombi lake kwa mahakama, Bw Mwau anasema kuwa hatua ya NPSC kuanzisha mchakato wa uajiri ni kinyume cha Katiba, kwani ni Inspekta Jenerali pekee aliye na mamlaka ya kuongoza masuala ya ndani ya huduma ya polisi.
Mahakama iliagiza mawakili wa Bw Mwau kuwakabidhi stakabadhi za kesi washitakiwa wote, wakiwemo Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja, Huduma ya Polisi (NPS), Tume ya Kitaifa ya Polisi (NPSC), na Mwanasheria Mkuu Dorcas Oduor.
Kesi hiyo itatajwa tena Oktoba 21 ili kuthibitisha iwapo pande zote zimezingatia maagizo ya mahakama na kuwasilisha hoja zao rasmi.
Bw Mwau anadai kuwa NPSC imejaribu kwa njia isiyo halali kuvamia mamlaka ya Inspekta Jenerali kwa kuendesha zoezi la uajiri bila idhini ya kikatiba. Anaonya kuwa kuendelea na mchakato huo kunaweza kuwahusisha maelfu ya raia katika zoezi ambalo kisheria litakuwa limekiuka Ibara ya 2 ya Katiba.
Kwa mujibu wa Bw Mwau, NPSC sio chombo cha usalama wa kitaifa na hivyo haiwezi kuendesha uajiri chini ya Ibara ya 238(2)(d) ya Katiba.
“Katiba iko wazi, uajiri wa maafisa ni jukumu la chombo cha usalama wa kitaifa, ambacho katika kesi hii ni Huduma ya Polisi. Kwa hivyo, hatua ya mshtakiwa wa tatu (NPSC) kuendesha zoezi hili ni kinyume cha katiba na batili kulingana na Ibara ya 2(4),” alisema.
Aliongeza kuwa Ibara ya 245(4) ya Katiba inakataza mtu yeyote au taasisi yoyote kuingilia mamlaka ya Inspekta Jenerali kuhusu masuala ya uajiri wa maafisa wa polisi, jambo linalosisitiza uhuru wake katika uongozi wa huduma hiyo.