KPAWU, Delmonte zatia saini CBA ya kuimarisha maslahi ya wafanyakazi
MUUNGANO wa Wafanyakazi katika Sekta ya Upanzi na Kilimo (KPAWU) Jumanne ulitia saini Mkataba wa Maelewano (CBA) na Del Monte Kenya ambao utadumu kwa miaka miwili (2025-2027).
Makubaliano hayo yalitiwa saini mbele ya Katibu Mkuu wa Muungano wa Wafanyakazi Nchini (COTU) Francis Atwoli, Naibu Katibu Mkuu wa KPAWU Thomas Kipkemboi na uongozi wa matawi unaowawakilish wafanyakazi kwenye kampuni ya Del Monte.
Kampuni hiyo iliwakilishwa na Meneja Mkurugenzi Wayne Cook na Mkuu wa wafanyakazi Gideon Kimutai.
Makubaliano hayo ya CBA yalipisha nyongeza ya asilimia sita hadi tisa kwa wafanyakazi 7,000 wa Del Monte.
Bw Atwoli alisifu hatua hiyo akisema kuwa inaonyesha kuna nia ya kuimarisha maslahi, mapato na maisha ya wakulima.
Pia usimamizi wa Del Monte ulihakikishia KPAWU kuwa wafanyakazi watanufaikia nyongeza ya marupurupu ya nyumba pamoja na kunufaikia bima ya matibabu na manufaa mengine ya kielimu.
Bw Atwoli alisifu uongozi wa Kampuni ya Delmonte na KPAWU kwa kuandaa mazungumzo na kuelewana kuhusiana na vigezo vyote huku akionyesha imani yake kuwa sekta ya kilimo itaendelea kupiga hatua.
“Kama KPAWU tunahakikishia usimamizi wa Del Monte kuwa mradi tu wanazingatia maslahi ya wafanyakazi wao, tutaendelea kuwaunga ili mapato yao yaongezeke ndipo wafanyakazi nao wanufaike zaidi,” akasema Bw Atwoli.
Bi katibu huyo wa Cotu ambaye pia anashikilia wadhifa huo kwenye KPAWU, alisema muungano huo unamakinikia kupigania maslahi ya wakulima katika sekta yote.
Alisema juhudi na nguvu kazi za wakulima lazima zichangie wao kuishi maisha mazuri.